Friday, September 22, 2017

DC, KILWA" AZIPIGIA MAGOTI TAASISI ZA FEDHA ZIWAHURUMIE WENYE VIPATO VIDOGO

Na.Ahmad Mmow. 
LICHA ya kuhaidi kuvitafutia mikopo vikundi wajasirimali vilivyopo katika wilaya yake. Mkuu wa wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi,Christopher Ngubiagai ametoa wito kwa taasisi za fedha zinazotoa mikopo  kuwahurumia watu wenye vipato vidogo kwa kulegeza masharti na kupunguza viwango vya riba. 

Ngubiagai anaetambulika kwa jina la Komredi alitoa wito huo wakati anafungua semina ya wajasiriamali iliyofanyika leo katika mamlaka ya mji mdogo wa Kilwa Masoko.Semina ambayo iliandaliwa na mamlaka ya mapato nchini (TRA) mkoa wa Lindi. 

Alisema tasisi za fedha zinanafasi na uwezo mkubwa wakuisaidia serikali katika mkakati wake wa kuwainua wananchi wake wenye vipato vidogo ili waweze kushiriki kikamilifu ujenzi wa uchumi wa nchi kwa kulegeza baadhi ya masharti na viwango vya riba. 

Mkuu huyo wa wilaya huku akionesha kuhuzunishwa na kuguswa na changamoto wanazokutananazo wajasiriamali,alisema kutokana na masharti magumu na viwango vya riba vilivyopo kwenye baadhi ya benki zinasababisha wakopaji kukosa amani na kuishi kwa hofu badala ya kufurahia mikopo wanayokopeshwa. 

"Zipo taasisi na benki chache ambazo siwezi kuzitaja,zinamasharti na riba nafuu.Lakini ziponyingine ambazo pia sitazitaja,ukikopa unakosa amani,unakosa furaha na unakonda kama unanyonywa damu na jini.Siwezi kuziagiza zilege masharti na riba bali ziwahurumie wenyevipato vidogo," Komredi Ngubiagai aliomba na kusisitiza kwa njia ya utani. 

Kuhusu azima ya kuvitafutia mikopo vikundi vya ujasiriamali,mkuu huyo wa wilaya alisema kwanafasi yake atahakikisha vinapata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha zenye masharti na riba nafuu.Huku akiwahakikishia wajasiriamali hao kwamba taasisi hizo zipo na ameanza kufanyanazo mazungumzo kuhusu hilo.

Mbali na hayo,alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kupokea na kuyafanyia kazi mabadiliko,badala ya kusubiri madiliko yawabadidishe.Ikiwemo kuwa na malengo mahususi katika shuguli zao. 
" Katika dunia ya leo huwezi kufanya shuguli yoyote bila elimu ukatarajia mafanikio.Hata hivyo sekta isiyorasimi inamchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi yoyote duniani,hakuna serikali iliyoweza kuwaajiri wananchi wake wote.Nawaagiza maofisa maendeleo wapeni mafunzo," alisema. 

Kwa upande wake ofisa wa TRA wa kitengo cha elimu kwa walipa kodi wa mkoa wa Lindi,Odupoi Papaa,licha ya kueleza mikakati ya serikali ya kuwainua wafanyabiashara wadogo.Ikiwamo kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria za kodi. 

Aliwaasa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla kupeleka malalamiko na ushauri kwenye ofisi zacmamlaka hiyo ili yafanyiwe kazi. 

Habari Ahmed: Alisema mamlaka hiyo  ipo kwaajili ya kuwahudumia wananchi.Kwasababu nitaasisi ya serikali ya wananchi wenyewe.Hivyo maofisa wa idara hiyo niwatumishi wao.

MAWAKILI WA UINGEREZA WAMTAKA MAGUFULI KUANZISHA UCHUNGUZI KUHUSU LISSU

Chama cha mawakili na watetezi wa haki za kibinaadamu nchini Uingereza wamemuandikia barua rais John Pombe Magufuli kikimtaka kuanzisha uchunguzi ulio huru mara moja kuhusu jaribio la mauaji lililotekelezwa dhidi ya mbunge wa Singida mashariki Tundu Lissu. 

Wakili huyo ambaye pia ni rais wa chama cha mawakili nchini Tanzania TLS mnamo tarehe 7 mwezi Septemba alipigwa risasi tumboni na miguuni na watu wasiojulikana katika makaazi yake ya Dodoma. 

''Ufyatulianaji huo wa risasi na maswala mengine ambaye yemetokeo yanayowahusisha mawakili yanatia wasiwasi''. 

Ni muhimu mkubwa kwamba chama cha mawakili kinaheshimiwa kwa kuwa ni kitengo muhimu katika kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa kikamilifu, ilisema barua hiyo. 

Barua hiyo ilisainiwa siku ya Jumatano na rais wa chama cha mawakili Joe Egan ,mwenyekiti wa baraza hilo Andrew Langdon na Mmwenyekiti wake Kirsty Brimelow. 

Mawakili hao wamemwambia rais Magufuli pia kuanzisha uchunguzi kuhusu visa vyengine vya uhalifu vinavyotekelezwa dhidi ya mawakili. 

Visa hivyo ni pamoja na mlipuko katika afisi ya mawakili ya IMMMA chini ya mwezi mmoja na tisho la waziri wa maswala ya kikatiba na sheria Harrison Mwakyembe la kutaka kufutilia mbali chama cha mawakili nchini Tanzania katika kipindi cha miezi saba iliopita. 

Tuesday, September 19, 2017

SABABU TISA ZA KIAFYA KWANINI UNATAKIWA KUTUMIA ZABIBU KILA WAKATI


Kwa mujibu wa tafiti za kiafya zinaonyesha, ipo faida kubwa sana kwa mtu yeyote anayetumia zabibu katika upande wa afya yake. 

Inaonyesha moja kwa moja, zabibu kutokana na wingi wa madini zilizonayo ndani yake, zina uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali kama zikitumiwa kwa uhakika. katika makala haya tumekuwekea dondoo za kukusaidia kukuonyesha baadhi ya magonjwa yanaweza kutibiwa au kuepukwa hasa kutokana na matumizi ya zabibu. 

1. Zabibu inatibu pumu (Asthma) 
2. Zabibu ina imarisha mifupa. 
3. Zabibu inazuia magonjwa mengi ya moyo. 
4. Zabibu inapunguza unene kwa sehemu. 
5. Zabibu inapunguza kisukari. 
6. Zabibu ni kinga ya magonjwa ya meno. 
7. Zabibu ni kinga kwa kansa ya matiti. 
8. Zabibu inapunguza ugonjwa wa mapafu. 
9. Zabibu inapunguza tatizo la kushindwa kuona mbali.

ZALISHA MATANGO UBORESHE KIPATO KWA MUDA MFUPI


Hili ni zao la biashara, pia chakula. Zao hili hustawi na kulimwa kwa wingi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Pwani. 

Matumizi:   Matango hutumika kama tunda, ijapokuwa ni aina ya mboga na huongeza vitamin A, C na maji mwilini. Pia, tango linaweza kutumiwa kama saladi wakati wa mlo. 

Hali ya hewa:  Matango hustawi kwenye hali ya joto, hali kadhali kwenye sehemu yenye joto kidogo pia hustawi. Matango yanahitaji joto wastani wa nyuzi joto 20°C – 25°C. Zao hili pia huhitaji maji kwa wingi, ingawa unyevu ukizidi husababisha magonjwa kwenye majani na maua. 

Udongo:   Kwa ustawi mzuri wa matango, udongo unatakiwa kuwa na rutuba ya kutosha, na chachu ya kuanzia 5.5 hadi 6.7, mwinuko unaotakiwa ni kuanzia mita 1000-1200 kutoka usawa wa bahari. 

Tofauti na ilivyo mazao mengine, matango hayahitaji mwanga mkali sana kwa kuwa husababisha maua dume kuzaliwa, hivyo kuathiri uzalishaji wa idadi ya matunda ya matango. Mwanga kidogo husababisha maua jike kuchanua kwa wingi kuongeza kiwango cha mazao. Mwanga unapokuwa mwingi, inabidi kutumia neti au aina nyingine ya vizuizi ili kupunguza mwanga, ambapo pia itasaidia kulinda mmea dhidi ya upepo mkali ambao unaweza kuharibu maua na matunda, au mmea kwa ujumla. 

Kupanda:  Mara nyingi matango hupandwa moja kwa moja shambani. Wakulima wengine hupanda kwenye vitalu au makopo na baadae kuhamishia miche inapofikia sentimita 8-12. Endapo mbegu zimepandwa shambani moja kwa moja, inatakiwa ipunguzwe na kubakia mche mmoja tu kwenye kila shimo. 

Nafasi:  Nafasi kati ya mche na mche ni sentimita 60-70, na nafasi kati mstari na mstari ni sentimita 70-90. Mimea inatakiwa iwekewe miti ili iweze kuzaa matunda mengi na kuepuka kukaa chini ambapo matunda yanaweza kuoza au kuharibiwa na wadudu. 

Mbolea:   Mbolea ni muhimu sana, kabla ya kupanda au kuhamisha miche. Mbolea inayoweza kutumika ni samadi au ya viwandani isiyokuwa na madhara kwa mazingira na afya ya binadamu. Baada ya kupanda, tumia mbolea ya maji maji kila baada ya siku 14-21, mpaka mmea uweke matunda. 

Palizi:  Palizi ni muhimu , ili kuepuka magonjwa na kunyang’anyana chakula kati ya zao na magugu. 

Wadudu waharibifu:  Wadudu waharibifu wa matango ni pamoja na Vidukari, inzi weupe, na minyoo ya mizizi. 

Magonjwa:  Magonjwa yaliyozoeleka kushambulia matango ni pamoja na Ukungu, fusari, na magonjwa ya virusi. 

Kuvuna:   Matango yanaweza kuwa tayari kuvunwa kuanzia siku 50-60 na matunda yanatakiwa yawe na urefu wa sentimita 15 mpaka 20. Makadirio ya mavuno ni tani 6 kwa ekari moja.

WEKA PEMBENI TABIA HIZI, UJENGE MAISHA YA MAFANIKIO UNAYOYATAKA


Je, uko tayari kufanikiwa kwa namna yoyote ile? Je, kuna changamoto unazopitia na zinakuzuia kufanikiwa, ingawa wewe kiu yako ni kutaka kuona mafanikio yakiwa kwenye maisha yako? Endapo utamuuliza mtu yeyote swali hili, wengi sana watakwambia, ndio wanataka kufanikiwa, tena utajibiwa kwa haraka sana. 

Lakini hata hivyo ni kweli, karibu kila mtu katika maisha yake ana kiu ya kufanikiwa lakini si kila mtu anajua jinsi ya kufanya ili kufanikiwa. Kuna vitabu vingi vimeandikiwa, na makala nyingi zimeandikwa zikieleza kwa wazi nini unapaswa kufanya ili kufanikiwa, na nini ambacho unatakiwa kuepuka sana ili kufanikiwa. 

Pamoja na wingi wote wa vitabu na makala hizo za mafanikio, lakini bado watu hawafanikiwi, wamekuwa ni watu wa maisha yale yale, mpaka unaweza ukaa chini ukajiuliza hivi, shida kubwa ipo wapi? Leo kupitia makala haya, nataka nikukumbushe kwa kifupi sana, baadhi ya tabia unazotakiwa uziweke pembeni ili ufanikiwe. 

Zifuatazo ni baadhi ya tabia ambazo  

1. Ubinafsi. 
Sumu mojawapo kubwa katika biashara na mafanikio kwa ujumla ni ubinafsi. Haitakiwi kuwa mbinafsi unapokuwa kwenye biashara, inatakiwa kutoa ushirikiano na kwa wengine ili mafanikio yako ya kibiashara yaweze kukua. Ukiwa mbinafsi, utakosa ushirikiano kwa wengine na utakwama. 

2. Hofu. 
Hutaweza pia kufanikiwa kama kila wakati kama una hofu kubwa kwenye kila kitu unachotaka kukifanya. Hofu zako zote ulizonazo, zitupe kule. Hofu ni sumu na kizuizi kikubwa sana cha mafanikio yako. Hata hivyo kila mtu ana hofu, lakini hofu zako pia unatakiwa kuzishinda hadi kuchukua hatua kwenye ndoto zako. 

3. Uvivu 
Je, umeshawahi kukutokea asubuhi ambapo kunapokucha unakuwa unajishauri uamke au usiamke, ndani yako kuna kuwa na mabishano mengi sana ya nini ufanye? Kama hali hiyo ilishawahi kukutokea basi ni dalili mojawapo ya uvivu, ambapo ni kitu kimojawapo unachotakiwa kukitupa kule ili uweze kufanikiwa. 

4. Hisia hasi. 
Kuendelea kuwa na hisia hasi, wakati unatafuta mafanikio, huko ni kujitafutia balaa la kushindwa kwenye maisha yako. Hisia hasi ni mbaya katika biashara yako, hisia hasi ni mbaya katika maisha yako pia. Zinakufanya ushindwe kufanya mambo yako kwa ufasaha nakujiona kuwa ni mtu kama wa visasi, ziepuke hisia hizi ili ufanikiwe. 

5. Waepuke watu hasi sana. 
Kama unataka kuwa na mafanikio, epuka sana watu hasi, watu ambao wanaweza kuwa sumu kubwa kwenye maisha yako. Watu hawa hawawezi kukusaidia kitu chochote zaidi watakurudisha nyuma kutokana na maneno yao, kutokana na hisia  zao. Wakimbie watu hawa ili utengeneze mafanikio yako.

MGOGORO GEITA NGOMA BADO TETE

Mgogoro kati ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na baraza la madiwani wa halmashauri mbili za Geita umechukua sura mpya, baada ya kikao cha kutafuta suluhu kukwama kutokana na mahudhurio hafifu.

Septemba 14, uongozi wa Mkoa wa Geita uliwataka madiwani waliofunga barabara za kuingia GGM kuwa watulivu kusubiri kikao na kamishna wa madini.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi alisema wamekubaliana kuahirisha kikao hicho hadi madiwani wanaoshikiliwa polisi watakapofikishwa mahakamani na kupata dhamana, ndipo waitishe kikao maalumu atakachoshiriki pia kamishna wa madini nchini.

Madiwani 10 akiwamo Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma wanashikiliwa na polisi wakiwemo wananchi watano na Katibu wa Vijana wa CCM wa Wilaya ya Geita, Ally Rajabu.

Kushikiliwa kwao kunatokana na vurugu zilizotokea Alhamisi iliyopita kwa madiwani kudaiwa kufunga barabara zinazoingia GGM wakishinikiza kulipwa Dola 12 milioni za Marekani (zaidi ya Sh26 bilioni zinazotokana na ushuru wa huduma kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.

Kamishna wa madini nchini, Benjamin Mchwampaka jana alisema baada ya kumalizika kikao kilichohudhuriwa na kamati za ulinzi na usalama za mkoa na wilaya na ofisi ya madini ya mkoa kuwa hawakuendelea na kikao kingine kutokana na madiwani kutohudhuria.

Mchwampaka alisema lengo la kufika Geita ni kutafuta muafaka baina ya pande hizo lakini imeshindikana kutokana na baadhi ya madiwani kushikiliwa na vyombo vya dola na wengine kutohudhuria kikao hicho.

Madiwani hao wanasema fedha wanazoidai GGM ni haki yao kwa mujibu wa sheria kwa kuwa mgodi ulipaswa kulipa ushuru wa huduma wa asilimia 0.3 lakini hawakulipa na badala yake walilipa Dola 200,000 kwa mwaka tangu 2004 hadi 2013 kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Jamii wa GGM, Manase Ndoroma alisema kinachosababisha mgogoro kati ya pande hizo ni kupingana kwa sheria ambazo zote zimetungwa na Bunge.

Alisema sheria ya madini iliwaruhusu kulipa Dola 200,000 kwa mwaka, huku sheria ya baraza la madiwani ikiwa imepitisha malipo ya asilimia 0.3 jambo linalosababisha mgogoro na suluhisho pekee ni kwenda mahakamani.

LIMETOLEWA AGIZO LA KUKAMATWA WAUAJI

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama Mkoani humo kuwasaka watu wote waliohusika katika jaribio la mauaji ya watu wanne ambao walipigwa na kuwachoma moto katika kijiji cha Mwanabondo, Wilayani Uyui Mkoani humo kwa tuhuma za ushirikina.

Mwanri amesema kuwa vitendo vya wananchi kuendelea kujichukulia sheria mikono havivumiliki na havikubaliki hata kidogo kwa kuwa vyombo vya sheria vipo ambavyo vinaweza kutekeleza majukumu yake.

Mkuu huyo wa Mkoa ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa amesema licha ya tukio hilo kutokea lakini sio la kwanza hivyo vyombo vya usalama lazima vihakikishe vinawatia nguvuni watu wanaotekeleza matukio hayo.

Wakiongea wakiwa Hospitali Mkoani humo baadhi ya wahanga wa Tukio hilo wamesimulia jinsi walivyotaka kuuawa na watu hao wasiojulikana ambao walitokomea mara baada ya kushindwa kutekeleza azma yao.

KUTANA NA KIJANA WA MIAKA 17 ALIYETENGENEZA SIMU

Mo Omer anatarajia kuuza zaidi simu alizotengeneza katika mataifa hasa ya Afrika

Kijana wa miaka 17 kutoka nchini Canada ambaye alijitengenezea mwenyewe simu baada ya mama yake mSomali kusema kuwa hana uwezo wa kumnunulia simu ya smartphone amezungumza na BBC.

Mo Omer - ambaye anajiita mwenyewe "tech nerd" - alitengeneza simu ya smartphone kuanzia mwanzo , na anasema ataiuza kwa dola $180.

"Ina kila kitu unachoweza kukipata katika simu ya kawaida, ni kwamba tu haina gharama kubwa ," ameiambia BBC.

Simu "sio vifaa vigumu kutengeneza", aliongeza- na akasema ana azma ya kuzipeleka katika baadhi ya maeneo ya Afrika.

"Tumepokea maombi kutoka Nigeria na Algeria na maeneo mengine mengi. Ni soko linalokua kwa kasi ambalo tungependa kuingia ".

BBC

KILICHOFANYA UTETEZI WA MANJI KUSOGEZWA HADI SEPT 25

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, 'imepiga kalenda' kusikiliza ushahidi wa utetezi wa kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin inayomkabili mfanyabiashara Yusufally Manji.

Kesi hiyo 'imepigwa kalenda' baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis kuwa na udhuru wa kikazi na Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayeisikiliza kuridhia ombi la Jamhuri.

Vitalis alidai jana kesi hiyo, ilipangwa kuendelea na ushahidi wa utetezi, lakini amepata udhuru wa kikazi na kuomba tarehe nyingine ya kuendelea.

Hakimu alisema kesi hiyo itasikilizwa mfululizo kuanzia Jumatatu mpaka Jumatano ijayo.

Kabla ya kupangwa tarehe nyingine ya kusikiliza kesi hiyo, hakimu alimuonya Manji kwa kuchelewa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake.

Manji alidai kuwa aliwasiliana na wakili wake kwasababu alikwenda hospitali na kwamba tukio hilo halitajirudia tena.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu eneo la Upanga Sea View, jijini Dar es Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

UCHAGUZI KENYA KUAHIRISHWA

UCHAGUZI wa marudio wa urais nchini Kenya huenda ukaahirishwa kutoka tarehe 17 mwezi ujao.

Tume ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, imekuwa ikikutana kuangalia uwezekano wa kuahirisha Uchaguzi huu baada ya kampuni ya Ufaransa ya Safran Morpho kuomba muda zaidi kuboresha mitambo inayotumiwa kuwatambua wapiga kura.

Mbali na hilo, Muungano wa Upinzani Nasa, unaoongozwa na Raila Odinga, umesema Uchaguzi hautafanyika iwapo marekebisho hayatafanyika ndani ya Tume ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na kujiuzulu kwa Ezra Chiloba Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo.

Chama cha Jubilee cha rais Uhuru Kenyatta kinashutumu shinikizo hilo la upinzani na kusisitiza uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa.

Saturday, September 9, 2017

JINSI UNAVYOWEZA KUWA SUMAKU YA FEDHA, NJIA 10 ZA KUIVUTA FEDHA IJE KWAKO MUDA WOTE

Linapokuja swala la fedha, kila mtu ana hisia tofauti, na hisia hizi zinatokana na malezi ambayo tumepata kwenye jamii ambazo tumekulia. Na katika hisia hizi, nyingi huwa ni hasi, kwamba fedha ni kitu kibaya au kitu ambacho hakihitaji kujadiliwa mara kwa mara. 

Kwa kusoma tu hiko kichwa cha habari kwamba kuna namna unaweza kuwa sumaku ya fedha, kuna watu tayari wameshakuwa hasi, kwamba kwa nini huyu Makirita anaandika kuhusu fedha, kwanza yeye anazo kiasi gani, na mengine mengi. Nakuelewa kama wewe ni mmoja wa watu wenye hisia hizi hasi, kwa sababu halikuwa kosa lako kuwa nazo, ila kama utasoma hapa mpaka mwisho na ukaendelea kuwa na hisia hizo, hapo sasa ni kosa lako. 

Tutakachokwenda kujifunza hapa ni kwamba wewe unaweza kuivuta fedha ije kwako, na kwa njia za kawaida kabisa, wala sio kwa nguvu ambazo hazieleweki kama wengi wanavyodanganyana. Zipo njia zilizodhibitishwa kisayansi ambazo zinafanya kazi kwa watu wote bila ya kujali kiwango cha elimu, rangi, au unatokea familia gani. 

Nina hakika umewahi kusikia usemi kwamba mwenye nacho huongezewa, ya kwamba tajiri ataendelea kuwa tajiri na masikini ataendelea kuwa masikini. Huu ni usemi uliowekwa na watu walioliona hilo likiendelea kwa wengi, lakini wakashindwa kulichimba kwa undani. Ukweli ni kwamba tajiri anaendelea kuwa tajiri kwa sababu ameshakuwa sumaku ya fedha, anajua jinsi ya kuzivuta zije kwake. Na masikini anaendelea kuwa masikini kwa sababu hajaijua mbinu ya kuzivuta fedha zije kwake. Je unataka kuzijua mbinu za kuvutia fedha zije kwako? 

Karibu tujifunze mambo haya kumi unayoweza kuanza kufanya leo kwenye maisha yako na ukazivutia fedha kuja kwako. 

1. Kuwa mkarimu, wasaidie wengine kwa chochote unachofanya. 
Njia ya kwanza kabisa ya kuzivutia fedha kuja kwako ni kuwa mkarimu. Chochote kile ambacho unakifanya kwenye maisha yako, iwe kazi au biashara, hakikisha lengo la kwanza ni kuwasaidia watu. Unawasaidia watu kwa kuwapa huduma ambazo ni bora na zinawaondolea maumivu wanayopata sasa au kuwapatia mahitaji wanayokosa sasa. 

2. Kuwa na shukrani kwa fedha ulizonazo. 
Haijalishi ni fedha kiasi gani unapata, hata kama ni kidogo sana, kitu muhimu kabisa ni kushukuru. Shukuru kwamba umepata nafasi ya kupata kiasi hiko cha fedha, ukijua ya kwamba kuna wengine wengi ambao hawajapata nafasi kama yako. Ukikutana na shilingi mia njiani wakati unapita, iokote kwa furaha. 

Unapokuwa mtu wa shukrani unakaribisha zaidi kile ambacho unashukuru. Wengi huwa walalamikaji kwa fedha kidogo wanazopata na hapa wanafukuza zaidi nafasi yoyote ya kupata zaidi. Kuwa mtu wa shukrani, utavutia fedha nyingi zaidi. 

3. Usiwaonee wivu wengine. 
Kama kuna watu wengine wenye fedha nyingi kuliko wewe, usiwaonee wivu, badala yake wabariki. Mafanikio ya wengine siyo sababu ya wewe kushindwa. Na unapojenga wivu dhidi ya wengine unaiambia akili yako kwamba kuwa na fedha siyo kitu kizuri na hivyo inazikimbia fursa za fedha. Lakini unapowabariki wale wenye fedha kuliko wewe, unaifungua akili yako na kuziona fursa nyingi zaidi za kifedha. 

4. Usijione mwenye hatia kwa kuwa una fedha nyingi. 
Moja ya vitu vinavyowafanya wengi kutokuvutia fedha ni kujiona kama wakiwa na fedha nyingi basi wale wanaowazunguka hawatajisikia vizuri. Huku ni kujiona mwenye hatia kama utakuwa na fedha. Na kujiona mwenye hatia kutaiambia akili yako iepuke mazingira yoyote yanayoweza kukuletea fedha zaidi. Jione kuwa wa msaada kama utakuwa na fedha nyingi zaidi, na utazivutia zaidi na zaidi. 

5. Kuwa na mapenzi makubwa kwenye kile unachofanya. 
Chochote unachofanya kwenye maisha yako, jambo muhimu kabisa ni ukipende sana. Penda kile unachofanya. Kuna usemi unasema kama kazi yako ni kitu unachopenda, hutafanya kazi kwenye maisha yako. Na mwingine fanya kile unachopenda na fedha haitakuwa tatizo kwako. Fanya kitu unachopenda kufanya, iwe ni kazi au biashara, na weka moyo wako wote kwenye kitu hiko na hakuna kitu kinaweza kukuzuia wewe kupata fedha zaidi. 
Wengi wamekuwa wakifanya vitu ambavyo hawavipendi ili tu wapate fedha, na wanashangaa kwa nini hawazipati, jibu ni kwa sababu wanazifukuza wao wenyewe. Unapofanya unachopenda, unazivutia fedha kuja kwako. 

6. Ukipoteza fedha, usijione mnyonge na kulalamika. 
Pale unapopoteza fedha, na lazima utapoteza iwe ni kwa hasara au kudhulumiwa, usianze kulalamika kwa nini inatokea kwako tu, bali jifunze ni nini kimepelekea wewe kufikia kwenye hali hiyo. Na hakikisha hurudii tena makosa ambayo uliyafanya awali na yakakufikisha hapo. Labda unahitaji kuwa makini zaidi, labda unahitaji kuangalia wale unaowaamini na mengine mengi. 
Ukiishia tu kulalamika na kuona wewe huna hatia, utaendelea kurudia makosa yale yale na kamwe hutazivutia fedha kuja kwako. 

7. Siku zote timiza ahadi zako. 
Fanya kile ambacho umeahidi utafanya, na kikamilishe kwa wakati na kwa ubora. Usiwe mtu wa kuahidi kwa maneno na wakati wa matendo huonekani. Timiza ahadi zako na utavutia fedha nyingi zaidi kwako. Iwe ni kwenye kazi au kwenye biashara, unachomwahidi mwajiri wako kitimize, na hatakuwa na jinsi bali kukuthamini zaidi. Chochote unachomwahidi mteja wako timiza, na atapata huduma bora zitakazomfanya awe mteja wako wa kudumu na kuwaambia wengine wengi zaidi. 

8. Tegemea kuwa tajiri. 
Haijalishi maana yako ya utajiri ni nini, tegemea kuwa tajiri. Na usiishie tu kutegemea bali kuwa na mpango kabisa wa jinsi gani utafikia utajiri wako, kipato chako kiwe kiasi gani, uwekeze kiasi gani ili uweze kufikia utajiri. Utajiri hauji kama ajali, ni zao la malengo, mipango na juhudi kubwa. Kama hutegemei kuwa tajiri huwezi kuvutia fedha kwako. 

9. Amini kwenye wingi. 
Kuna fedha nyingi sana kwenye dunia hii, nyingi mno, japo wengi wanakushawishi kwamba kuna uhaba wa fedha, siyo kweli. Amini kwenye wingi wa fedha na unachohitaji ni wewe kuja na wazo zuri la kuwasaidia watu na watakuwa tayari kukupa fedha zaidi na zaidi. Dunia haina uhaba wa fedha na mali, bali ina uhaba wa mawazo mazuri ya kuboresha maisha, njoo na mawazo mazuri na utavutia fedha zaidi na zaidi. 

10. Kuwa mkweli kwako, kuwa halisi. 
Linapokuja swala la fedha na utajiri, watu wengi sana sio wa kweli kwao binafsi na hata kwa wengine. Watu wengi sio halisi, bali ni feki, wengi wanaigiza maisha ya utajiri na wakati hali zao sivyo zilivyo. Wengi wanakazana waonekane kwa nje wana utajiri kumbe ndani yao mambo ni magumu. Watu wanaingia kwenye madeni makubwa ili tu kuonekana nao wapo. Hii sio njia nzuri ya kuvutia fedha zije kwako, badala yake utazikimbiza zaidi. Njia bora ya kuvutia fedha kuja kwako ni kuwa mkweli, na kuwa halisi. Ishi yale maisha ambayo ni yako, usitake kuleta maigizo, hakuna yeyote unayemfaidisha na badala yake unajiumiza mwenyewe. 

Hizo ndiyo njia kumi za kuzivutia fedha zije kwako na hatimaye uwe tajiri. Wote tunajua fedha ni muhimu, na kadiri unavyokuwa nazo nyingi inakuwa rahisi kwako kupata mahitaji ya msingi ya maisha yako, na hata kuwasaidia wengine pia. 

Njia zote hizi kumi zinaanza na wewe binafsi, haiangalii elimu yako ni kiasi gani, rangi ya ngozi yako, au kabila unalotokea. Pia haziangalii umri wako au umetoka familia ya aina gani. Ni wewe ufanye maamuzi leo na uanze kutekeleza hayo. Na ujue inachukua muda, siyo jambo la kutokea mara moja, hivyo kuwa mvumulivu. 

Neno la mwisho kabisa ninalotaka kukushirikisha ni kukuambia uchukue hatua, iwe utayafanyia haya kazi, au utayakataa na kuendelea na maisha yako ya sasa. Maamuzi ni yako wewe mwenyewe. Lakini jua hakuna mtu atakayekuja kukutoa hapo ulipo, utajitoa wewe mwenyewe.