Sunday, July 23, 2017

KISA CHA JUSTIN BIEBER KUPIGWA MARUFUKU CHINA


Nyota wa muziki wa Pop kutoka Canada Justin Bieber amepigwa marufuku kutumbuiza nchini China, kwa mujibu wa Wizara ya Utamaduni nchini humo.

Taarifa ya wizara hiyo imesema haifai kwa watumbuizaji ambao wamejihusisha katika "utovu wa nidhamu" kuruhusiwa kuingia nchini humo.

"Justin Bieber ni mwimbaji mwenye kipaji, lakini pia ni mwanamuziki kijana mwenye kuzua utata," amesema.

Taarifa hiyo imetolewa kujibu swali lililokuwa limeulizwa na mmoja wa watu katika tovuti ya wizara hiyo.

"Twatumai kwamba Justin Bieber atakapokomaa, anaweza kuendelea kuimarisha maneno yake na matendo, na kuwa mwanamuziki anayependwa kwa dhati na umma," taarifa hiyo imesema

Bieber aliwahi kuzuru China mwaka 2013, lakini sasa amejiunga na orodha ndefu ya wanamuziki waliopigwa marufuku nchini humo.

Wengine ni bendi ya Uingereza kwa jina Oasis na kundi la Marekani kwa jina Maroon 5, ambao wamepigwa marufuku kwa sababu ya misimamo yao ya kisiasa badala ya tabia.

Mwaka 2014, Bieber, maarufu kwa wimbo wake Sorry alizua utata baada ya kupakia picha aliyopigwa akitembelea madhabahu ya Yasukuni jijini Tokyo.

Madhabahu hayo nchini Japan yalijengwa kwa heshima ya wanajeshi waliouawa vitani pamoja na wahalifu wa kivita lakini nchini China na Korea Kusini, hutazamwa kama ishara kwamba Japan haijajutia makosa yaliyotendwa na watawala wa nchi hiyo China na Japan miaka ya nyuma.

No comments:

Post a Comment