Friday, August 26, 2016

DUDUBAYA AMFUNDISHA MWANAE KUVAA CONDOM

   Msanii Godfrey Tumaini au Dudubaya ameonesha mfano jinsi ya kuwa baba bora, kwa kuzungumza na mtoto wake kuhusu maambukizi ya magonjwa ya zinaa, na jinsi ya kujikinga na magonjwa hayo kwa kutumia condom.

      Akizungumza na Planet Bongo ya East Africa Radio, Dudubaya amesema huwa anazungumza na kijana wake kwa kuwa hataki apate magonjwa ya zinaa na kufa mapema kabla yake.

    "Mwezi wa 12 mwaka jana ndiyo nilikuwa naye alikuwa amefunga shule kwa hiyo kujiandaa kwenda form one, nilichomwambia siku moja mpaka washkaji walicheka maskani, nikamwambia dogo sikiliza, najua sasa hivi we unajisikia, sasa kama unajisikia unajua kuna kitu kinaitwa condom!? akaniambia yah, unajua kuitumia!?

       akasema hapana, nikamwambia unajua kuna magonjwa kama gono, kuna kaswende na UKIMWI, na sipendi utangulie wewe kufa mimi nikabaki, ni bora mimi nife wewe ndo uje kuwa mrithi wangu", alisema Dudubaya.

      Dudubaya aliendelea kusema kuwa wazazi wengi sasa hivi hawazungumzi na watoto wao na hatimaye watoto wanaingia kwenye mambo yasiyofaa, na mwisho wazazi huwalaum na kuwachukulia hatua watoto, kwa makosa ambayo wameyasababisha wenyewe.

   
     "Mtoto anapofikia kujisikia haina sababu ya kumfungia geti, na ndiyo maana unakuta kuna watoto wanapata maambukizi ya magonjwa kama UKIMWI, kumbe we mzazi hukuongea na mwanao, mzazi unatakiwa

     uzungumze na mwanao umwambie hivi na hivi, kwa mfano kama mjini hapa watoto kibao wanaharibika na madawa ya kulevya, kwa sababu mzazi huzungumzi na mtoto", Alisema Dudubaya.

Friday, August 19, 2016

VIGOGO WAWILI WA NIDA WAPATA DHAMANA

    VIGOGO wawili wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) wanaokabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.2 wameachiwa kwa dhamana. Washitakiwa hao ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani.

     Hata hivyo, washitakiwa wengine akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Dickson Maimu na wenzake watano wanaendelea kusota rumande.

      Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Respicius Mwijage alitoa uamuzi huo jana kwa kuwa washitakiwa hao wawili hawaguswi katika mashitaka yaliyofunguliwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi.

     Alisema anakubaliana na hoja za upande wa utetezi zilizowasilishwa na Wakili Johnson Jamhuri kuwa mashitaka yanayowakabili washitakiwa hao yana dhamana na hayahitaji kuombewa dhamana hiyo Mahakama Kuu.

     Hakimu Mwijage alisema, washitakiwa wanatakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya Sh mil 200, pia wawasilishe hati zao za kusafiria na hawatakiwa kwenda nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

MWILI. WA MTOTO WA ALBINO WAFUKULIWA KWA UCHUNGUZI

    MWILI wa mtoto mwenye albinism aliyefariki kwa maradhi hivi karibuni na kuzikwa Jumapili iliyopita, umefukuliwa chini ya ulinzi wa polisi ili ufanyiwe uchunguzi kutokana na kuibuka maneno yenye kutatanisha kuwa wakati akiugua alikuwa akivuja damu nyingi puani na kuvimba mwili.

     Mtoto huyo, Michael Juma aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu, alizikwa pembeni mwa nyumba yao Alhamisi wiki hii katika kijiji cha Bunambiyu, wilayani hapa na kuwashangaza wakazi wa eneo hilo.

  
      Katibu wa Chama cha Watu Wenye Albino Nchini (TAS), tawi la mkoa wa Shinyanga, Lazaro Anael alisema kitendo cha kuufukua mwili kimewashangaza na kwamba tangu taarifa za kifo cha mtoto huyo kujulikana, yamezuka maneno kuwa kifo hicho kina utata.

      Alisema alishiriki mazishi, lakini kabla ya kufika nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo akiambatana na Mkurugenzi wa Shirika la Under the Same Sun, Vicky Mtetema, waliukagua mwili wa mtoto huyo na kubaini haukuwa na tatizo.

     “Mimi nasema hivi maneno haya yanatoka wapi wakati mwili tuliukagua haukuwa na dosari yoyote wakati huo tulikuwa na Vicky Mtetema akiwa anaupiga mwili picha, viongozi wa kijiji na kata walikuwepo pamoja na majirani wakishuhudia kuwa salama na ndipo shughuli za maziko zilifanyika… sasa kitendo cha kufukua mwili hapo serikali inataka kuleta hofu,” alisema.

      Diwani wa Kata ya Bunambiyu, Richard Sangisangi aliyekuwa amekataa mwili huo kufukuliwa na kugoma kuwaita majirani kwa ajili ya kufukua mwili ili ufanyiwe uchunguzi aliondoka na kusema kamwe hawezi kuchuma dhambi kwa kile alichokieleza walishuhudia mwili ukiwa salama na alifariki kwa mapenzi ya Mungu sio ushirikina au kukatwa mapanga kama ilivyozoeleka maeneo mengine. Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jonathan Katela alisema kitendo cha kufukua mwili huo sawa na kurudisha majonzi kwa jamii na familia, lakini akasisitiza ameridhia kwa kuwa serikali imetaka mwili ufukuliwe kwa uchunguzi.

     Kauli kama hiyo ilitolewa na baba wa marehemu, Juma Masudi aliyesema ametii amri ya serikali, lakini yeye binafsi hakuridhika kuufukua mwili wa mwanawe aliyedai aliugua maradhi ya kawaida na kupata matibabu kituo cha afya Bunambiyu. Hata hivyo, baada ya mvutano,

    polisi walifanikiwa kufukua mwili huku Dk Hellen Kaunda aliyekuwepo eneo la tukio akiufanyia uchunguzi na kueleza haukuwa na dosari yoyote na kwamba alifariki kwa maradhi.

..... Msafara wa Polisi, Kitengo cha Upelelezi wilayani Kishapu kupitia msemaji wake kwenye eneo la tukio, Meshack Sumuni aliwaomba radhi wananchi na wazazi huku akiwatoa hofu kwa kitendo cha kufukua kaburi kuwa ni jambo la kawaida unapotoa utata.

SUMATRA YASEMA HAKUNA USAFIRI UTAKAOSITISHWA

    MAMLAKA ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) imewatoa hofu Watanzania kuhusu taarifa za kutokuwepo kwa huduma ya usafiri wa mabasi kwenda mikoani kuanzia Jumatatu na kusema kuwa inafuatilia kuhakikisha kuwa huduma hiyo inatolewa wakati wote.

     Pia, imesema maazimio yaliyotolewa na Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) kuhusu kufanyika kwa ukaguzi wa mabasi yote yaendayo mikoani Agosti 22, mwaka huu, usitishwe na kuwataka kutoa huduma hiyo hadi utaratibu maalumu utakapopatikana.

     Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe, alisema Taboa ilipeleka maazimio matatu yanayohusu ukaguzi wa magari unaolenga kuimarisha usalama na ubora wa huduma wanazotoa kwa jamii.

      Ngewe alisema mamlaka hiyo inakamilisha utaratibu huo wa kukagua magari pamoja na madereva na kwamba wanahitaji kuzungumza na taasisi inazoshiikiana nazo, ikwemo Kikosi cha Usalama Barabarani.

      “Maazimio haya ni mazuri na yanalenga kutoa huduma bora lakini hatuwezi kuanza ukaguzi Agosti 22 kwa kuwa tunahitaji vifaa kwa ajili ya kufanya ukaguzi huo na kujua ni mabasi yapi yataanza ukaguzi na yatakayofuata,’’ alisema Ngewe na kuongeza kuwa, wamiliki wa mabasi hayo pamoja na madereva wanatakiwa kufuata masharti ya leseni walizopewa kwa kusafirisha abiria hadi utaratibu rasmi wa ukaguzi utakapotolewa.

        Hata hivyo, alisema wananchi hawana budi kuondoa hofu ya kukosa usafiri kwakuwa hakuta utakaositishwa ili kupisha ukaguzi huo.

ARUSHA WATAKA MKUU WA MKOA AACHWE AFANYE KAZI

     WAKATI Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akiapishwa jana Ikulu, Dar es Salaam, baadhi ya wananchi wa Jiji la Arusha wameshangazwa kuona viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakidai kuwa anaingilia kazi za jiji hilo.

      Mkazi wa jiji hilo, Ismail Isaac alisema tatizo ni siasa za chuki kati ya Chadema dhidi ya RC Gambo na kutaka wamuache afanye kazi kwani wananchi wanamkubali, hivyo kama chama hicho cha upinzani hakimkubali, kitajua chenyewe.

       “Wananchi wanahitaji maendeleo sasa huu ushawishi wa Chadema kwenda kwa wenyeviti wa mitaa unatoka wapi? Huyu Gambo anafanya kazi, sasa vikwazo ni vya nini?” Alihoji Isaac na kusema kuwa Chadema inapaswa kutumikia wananchi na si maneno.

      Aidha, alimpongeza Rais John Magufuli kwa kumteua Gambo. Aliwashangaa madiwani wa Chadema wanaotaka siasa za chuki ambazo wananchi hawapo tayari kuzikubali.

      Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe, alisema Arusha kuna siasa nyingi hivyo ni vyema viongozi wakatimiza majukumu yao ya kikazi na kutokatishwa tamaa.

Wednesday, August 17, 2016

WABUNGE WOTE WANA HADHI SAWA-DK. TULIA ACKSON

    Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson Mwansasu amesema hakuna Mbunge ambaye ana hadhi ya juu kuliko mwingine katika Bunge, bali katiba inawatambua wabunge wote wapo sawa.

     Akizungumza katika mahojiano maalumu katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha ITV, Naibu Spika amesema makundi yote ya wabunge yakishaapishwa wote ni wabunge wanaofanana katika hadhi ya kufanya kazi wanapokuwa Bungeni.

       “Katiba ilivyoyaweka makundi matano ya wabunge kuanzia wanaoteuliwa na Rais, wanaochaguliwa na wananchi, wabunge wa viti maalum na wanaotoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wote wamewekwa kwa sababu maalumu kwa sababu hiyo wabunge wote ni sawa” Amesema Dkt. Tulia Aidha Naibu Spika ameitaka jamii kubadilika kutoka katika dhana kwamba mwanamke ambaye anashika nafasi ya juu katika uongozi kwamba amebebwa.

      “Wanawake wengi ambao wamepewa nafasi ya uongozi kwa kuchaguliwa au kuteuliwa ni mara chache sana hufanya vibaya na hata akifanya vibaya jamii humhukumu kwa kuwa ni mwanamke wakati kuna wanaume katika nafasi kama hiyo ambao pia unakuta wamefanya vibaya hivyo kuna changamoto hiyo katika jamii”

    Amesema Naibu Spika Dkt. Tulia. Kwa upande mwingine Naibu Spika Dkt. Tulia amesema anaongoza Bunge bila upendeleo wowote ila anafuata sheria na kanuni za kuongoza Bunge.

ARUSHA YAONGOZA KWA WIZI WA UMEME

   Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), limefanya ukaguzi wa miundombinu yake, kwa wateja 3,523 ambapo kati ya hao 165 walibainika kuibia shirika na kusababishia hasara ya zaidi ya bilioni 1.

    Akizungumza jana katika kijiji cha Seela Sing’isi, Wilayani Arumeru wakati wa ukaguzi wa miundombinu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa miundombinu Taifa, John Manyama, alisema ukaguzi huo wamefanya katika kipindi cha miezi tisa na kufanikiwa kupita mikoa 13 nchini.

      Manyama amesema katika mikoa hiyo 13, Mkoa wa Arusha unaoongoza kwa kuwa na wezi wengi wa umeme, ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza na Mbeya ni wa tatu, hali hii inawalazimu TANESCO wafanye ukaguzi wa mara kwa mara katika mikoa hiyo ili watu waache kuibia shirika la umma.

      Amesema katika maeneo ya Mererani kwenye migodi ya madini Tanzanite, kazi yao kubwa kuiba umeme, badala ya kutumia mita wanatumia 'cable' ili kuiba umeme, jambo ambalo pia ni hatari sana kwao na wafanyakazi wao.

      Manyama amesema wizi wa umeme unamadhara mengi kama kupoteza maisha kunakosababishwa na kukanyaga nyaya zinazofungwa kienyeji na wakati mwingine kusababisha nyumba kuungua.

     Amesema hakuna sababu ya wananchi kuiba umeme kwa sasa, kwani gharama zimeshuka kwa kiwango kikubwa, tofauti na siku za nyuma, hivyo ni vema kila mwananchi akafuata sheria kupata umeme halali.

       Naye Mhandisi Mkuu Mdhibiti Mapato TANESCO Makao Makuu, Poshelee Mwasenga amesema TANESCO walipoona kuna upotevu mkubwa wa umeme, ndipo walipoamua kuunda kamati hiyo maalum ya ukaguzi wa miundombinu na kukamata wezi wa umeme.

    Amesema Mkoa wa Arusha una tatizo kubwa kwa wizi wa umeme na eneo linaloongoza kwa wizi ni Meru, Wilayani Arumeru, wakifuatiwa na Mirerani kwenye migodi, jambo ambalo wao kama kamati wataendelea kufanya ukaguzi endelevu.

WAFUASI WA UPINZANI WAKAMATWA ZAMBIA

LUSAKA,

  POLISI nchini hapa wamewakamata watu 133 wanaopinga ushindi wa Rais Edgar Lungu, baada ya mshindani wake mkuu Hakainde Hichilema, kudai kuwa kura ziliibwa katika uchaguzi wa urais.

     Maandamano yalizuka katika sehemu nyingi za Mkoa wa Kusini ukiwemo mji maaarufu kwa utalii wa Livingstone. Mkuu wa Polisi Godwin Phiri, aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa waandamanaji walikuwa wakiwalenga wafuasi wa chama tawala na kisha kuharibu mali zao.

    “Ni mpango uliopangwa vyema na walikuwa wakisubiri mshindi atangazwe. Utulivu sasa umerejea kutokana na kufanyika kamata kamata,” aliongeza.

     Hichilema anasema kuwa ana mpango wa kupeleka kesi mahakamani kupinga matokeo hayo. Licha ya malalamiko ya upinzani kuhusu wizi na udanganyifu wa kura, Lungu alitangazwa na Tume ya Uchaguzi kutetea urais kwa kupata asilimia 50.35 katika uchaguzi wenye ushindani mkali ambao ulifanyika Alhamisi iliyopita.

    Mpinzani wake mfanyabiashara Hichilema kutoka Chama cha United Party for National Development (UPND) alipata asilimia 47.67 ya kura. Upinzani nchini umeishutumu Tume ya Uchaguzi (ECZ) kuingia makubaliano ya kumpendelea Rais Lungu na ameapa kupinga matokeo hayo katika Mahakama ya Katiba.

     Rais wa chama cha Movement for Multiparty Democracy MMD), Dk Nevers Mumba, amesema analo mkononi pingamizi la kuzuia matokeo yasitangazwe, jambo ambalo lilipuuzwa na tume.

     “Tulienda mahakamani Jumapili na tukapewa pingamizi la kuzuia ECZ isiendelee kutangaza matokeo ya uchaguzi na wakapuuza agizo la mahakama na kuendelea kutangaza kura zenye mgogoro,” alisema.

ALIYEDAIWA KUMUUA MKEWE KWA NYUNDO AKAMATWA

Shinyanga.  

    Jeshi  la polisi mkoani  Shinyanga linamshikilia mkazi  wa Kijiji  cha  Busongo  wilayani  Kahama  anayetuhumiwa kumuua  mke wake kwa kumpiga na nyundo kichwani kisha kukimbia baada  ya kutenda unyama huo.

     Kamanda wa  polisi  mkoani  Shinyanga  Muliro  Jumanne amesema kuwa wamemkamata mtuhumiwa  huyo ambaye anadaiwa kufanya  mauaji  ya Monica  Manyabhuluba   kisha  kutoweka  kukwepa  kunaswa  na mkono wa sheria.

     Mtuhumiwa  huyo ambaye alifanya mauaji  hayo Agosti  14 mwaka huu kisha kukimbia  amekamatwa leo akiwa Kahama mjini , baada ya taarifa kusambazwa maeneo mbalimbali  na wananchi  kutoa ushirikiano kwa polisi uliofanikisha kumtia mbaroni.

WALIOJERUHIWA NA MAJAMBAZI TABORA, WAFARIKI

   Kamanda wa Mkoa wa Tabora, Khamis Issah Sulemani.

     WATU wawili waliokuwa wamejeruhiwa kwa risasi wakati wa mapambano na majambazi katika kijiji cha Isila, wilaya ya Uyui mkoa Tabora, wamefariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora.

     Tukio hilo ambalo lilitokea usiku wa kuamkia juzi Jumapili ambapo majambazi watatu wakiwa na bunduki aina ya SMG, walivamia nyumbani kwa mfanyabiashara wa ng’ombe na kuwajeruhiwa kwa risasi watu wawili huku jambazi mmoja akiuawa wakati wa majibizano ya risasi na polisi na wengine wawili kutokomea kusikojulikana.

     Akithibitisha kutokea kwa vifo hivyo vya Bw. Mirija Bapa na ndugu yake Umoja Ubapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Khamis Selemani amesema kuwa watu hao walizidiwa ghafla wakati wakipata matibabu na kupeleka vifo vyao.

      Kamanda Selemani amesema kuwa Jeshi la Polisi bado linaendelea kuwasaka watuhumiwa wawili waliojeruhiwa na polisi katika tukio na kukimbia ambapo ametoa wito kujisalimisha wenyewe ili sheria ifuate mkondo wake.

SEMENYA KUSHIRIKI MBIO ZA MCHUJO LEO

   Mwanariadha wa Afrika Kusini Caster Semenya, hii leo atashiriki mbio zinazosubiriwa kwa hamu za mita 800 mchujo kwa akina mama.

      Utata umekumba taaluma ya Semenya tangu anafanyiwe uchunguzi wa jinsia yake mwaka 2009, ambapo aligunduliwa kuwa na viwango vya juu vya chembe chembe za kiume.

     Kabla ya kufanyika kwa mashindano ya olimpiki ya Rio, kulikuwa na maoni tofauti ikiwa Semenya angeweza kuruhusiwa kushiriki mbio za wanawake.

     Anatarajiwa kushinda mbio hizo na hata kuvunja rekodi ya miaka 33. Watu nchini Afrika Kusini wameingia kwenye mitandao ya kijamii kumtetea Semenya na hata kufikia kiwango cha kumtungia shairi.

Thursday, August 4, 2016

EVANS AVEVA AACHIWA KWA DHAMANA

      Huku Rais wa Simba, Evans Aveva akiwa ameachiwa kwa dhamana, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) imesema ilimshikilia kwa kuwa fedha dola 300,000 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Simba katika benki moja, kwenda kwenye akaunti na benki nyingine.

     Fedha hizo ni zile za malipo ya mwanasoka Emmanuel Okwi aliyeuzwa dola 319,212 lakini fedha hizo hazikulipwa mapema baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kufanya haraka katika mauzo hali iliyofanya uongozi wa Simba ulioingia madarakani kuanza kuhaha kupambana na Etoile hadi kufikia Fifa ili walipwe.

      Mkuu wa Uchunguzi wa Sekta ya Umma ya Takukuru, LEonard Mtalai amesema akaunti hiyo iliyohamishiwa dola 300,000 ni ya Aveva na baada ya hapo, dola 62,000 zilihamishwa kwenda Hong Kong na sasa Takukuru inashirikiana na wenzao wa nchini humo ili kujua kilichonunuliwa kupitia fedha hizo.

     Taarifa nyingine, zinaeleza fedha hizo dola 62,000 zilitumika kununua nyasi bandia ambazo tayari zimetua nchini kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mazoezi enero la Bunju na ujenzi umeanza.

     Ofisa huyo wa Takukuru, amethibitisha kuhojiwa kwa watu kadhaa pamoja na Aveva na kusema bado wanaendelea na uchunguzi. “Tutajitahidi kadiri ya uwezo wetu kuendelea na uchunguzi ili ukikamilika, kama tutagundua kuna matatizo basi mara moja sheria itafuata mkondo wake,” alisema.

     Awali, alieleza waliamua kuanza uchunguzi baada ya baada ya kupata taarifa za kiintelejensia kwamba kuna fedha nyingi zilihamishwa kutoka kwenye akaunti moja kutoka katika benki moja, kwenda akaunti nyingine katika benki tofauti.

    “Hii ilitufanya mara moja kuanza uchunguzi,” alisisitiza Mtalai.

"TIP TOP HATUISHI KIBOSI BOSI" MADEE

     Msanii Madee leo ameweka wazi mkanganyiko ambao wengi walikuwa nao kuhusu msanii anayemsimamia Dogo Janja, mbaye pia yuko chini ya Tip Top ambayo inamsimamia yeye Madee.

      Akiongea kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Madee amesema ingawa Dogo Janja yupo chini yake, lakini iwapo kuna kazi anatakiwa kuifanya, lazima afanye mawasiliano na Babu Tale, na kufikia uamuzi kwa pamoja, tofauti na wengi wakivyofikiri kuwa yeye ndio ana uamuzi na Dogo Janja.

       “Mtu akitaka collabo na Dogo Janja tunawasiliana na Babu Tale, na kama ishu ya kazi hawezi kukataa, lakini lazima tujadili, kwetu hatuishi kibosi bosi, kama ni jambo la msingi linawekwa mezani kila mtu anatoa maoni yake, kama afanye au asifanye”, alisema Madee.

      Madee ambaye pia alianza kwa kumtoa msanii Raymond mpaka akachukuliwa na wasafi ambako yuko sasa, amesema anajivunia mafanikio ya msanii huyo, kwani tayari yupo kwenye historia yake.