Wednesday, August 17, 2016

ARUSHA YAONGOZA KWA WIZI WA UMEME

   Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), limefanya ukaguzi wa miundombinu yake, kwa wateja 3,523 ambapo kati ya hao 165 walibainika kuibia shirika na kusababishia hasara ya zaidi ya bilioni 1.

    Akizungumza jana katika kijiji cha Seela Sing’isi, Wilayani Arumeru wakati wa ukaguzi wa miundombinu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa miundombinu Taifa, John Manyama, alisema ukaguzi huo wamefanya katika kipindi cha miezi tisa na kufanikiwa kupita mikoa 13 nchini.

      Manyama amesema katika mikoa hiyo 13, Mkoa wa Arusha unaoongoza kwa kuwa na wezi wengi wa umeme, ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza na Mbeya ni wa tatu, hali hii inawalazimu TANESCO wafanye ukaguzi wa mara kwa mara katika mikoa hiyo ili watu waache kuibia shirika la umma.

      Amesema katika maeneo ya Mererani kwenye migodi ya madini Tanzanite, kazi yao kubwa kuiba umeme, badala ya kutumia mita wanatumia 'cable' ili kuiba umeme, jambo ambalo pia ni hatari sana kwao na wafanyakazi wao.

      Manyama amesema wizi wa umeme unamadhara mengi kama kupoteza maisha kunakosababishwa na kukanyaga nyaya zinazofungwa kienyeji na wakati mwingine kusababisha nyumba kuungua.

     Amesema hakuna sababu ya wananchi kuiba umeme kwa sasa, kwani gharama zimeshuka kwa kiwango kikubwa, tofauti na siku za nyuma, hivyo ni vema kila mwananchi akafuata sheria kupata umeme halali.

       Naye Mhandisi Mkuu Mdhibiti Mapato TANESCO Makao Makuu, Poshelee Mwasenga amesema TANESCO walipoona kuna upotevu mkubwa wa umeme, ndipo walipoamua kuunda kamati hiyo maalum ya ukaguzi wa miundombinu na kukamata wezi wa umeme.

    Amesema Mkoa wa Arusha una tatizo kubwa kwa wizi wa umeme na eneo linaloongoza kwa wizi ni Meru, Wilayani Arumeru, wakifuatiwa na Mirerani kwenye migodi, jambo ambalo wao kama kamati wataendelea kufanya ukaguzi endelevu.

No comments:

Post a Comment