Biashara Nzuri Ambayo Unaweza Ukaifanya Na Kupata Faida Kubwa Ni Hii Hapa
Habari za leo, mpenzi msomaji wa safu hii ya biashara? Nikukaribishe kwa moyo mkunjufu ili tuweze kujifunza na elimu hii ya biashara. Andaa ubogo wako ili uweze kupokea mambo muhimu ya kukusaidi kufanikiwa.
Moja ya maswali ambayo nimekuwa nikiulizwa sana na wasomaji wetu ni kwamba je, afisa mipango Benson, nifanye biashara gani ambayo itakuwa ina faida kubwa kwangu?
Kama ambavyo nimekuwa nikiulizwa mara kadha wa kadha na swali hilo tena limekuwa likijirudia. Hivyo kwa kutumia dakika chache naomba niweze kujibu swali hilo.
Jambo la msingi sana ambalo unatakiwa kulizingatia ni kwamba kila biashara ambayo unaiona machoni mwako ina faida na hasara zake, Nimeanza kwa kusema hivyo kwani watu wengi wamekuwa wakiaangalia upande mmoja tu wa kupata faida tu.
Lakini ukweli ambao unatakiwa kuujua mapema ni kwamba kabla ya kuingia katika biashara tambua ya kwamba katika biashara hiyo kuna faida na hasara, hivyo uwe tayari kubeba mambo hayo mawili pindi yatakapojitokeza.
Biashara yenye faida huanza na wazo, wazo ambalo limekuwa likitokana na mfanyabiashara kabla ya kuanza kufanya biashara husika. Wazo hilo hujengwa na misingi ya kina ya kufanya uchunguzi yakinifu juu ya biashara hiyo.
Usipofanya uchunguzi wa kutosha juu ya biashara unayotaka kuifanya ipo siku utalalamika. Ila tunashauriwa ya kwamba katika kufanya uchunguzi wa kutosha ni lazima ujikite katika kuangalia eneo ambalo utaiendesha biashara hiyo.
Wakati unangalia eneo kwa ajili ya kufanyia biashara, angalia eneo ambalo:-
Eneo linalofikika kwa urahisi.
Angalia eneo ambalo lina uwingi wa mkusanyiko mwingi wa watu tofauti tofauti.
Tafuta eneo ambalo kuna upatikaji wa huduma za kijamii, kama vile ukaribu wa benki, umeme, maji na mengineyo mengi yatakoyokusiadia kukua kibiashara.
Angalia eneo ambalo lipo karibu na wafanyabiashara wengine. Kwa mfano, kama unafanya biashara ya mashati basi chagua eneo ambalo kuna mfanyabiashara anauza tai. Kufanya hivi kuna msaidia mteja kutopata tabu ya kuhangaika kupata bidhaa fulani.
Lakini kubwa kuliko yote ni kwamba katika kufanya uchunguzi wa eneo la kufanyia biashara ni vyema unafanya uchunguzi kwa kuangalia hasa ni yapi mahitaji ya watu.
Kisha wewe uweze kuyasogeza mahitaji hayo karibu.
Mwisho naomba ujiulize hivi, ni wapi ambapo imepanga kufanya biashara h? Na watu wana changamoto zipi nawe umekuja suluhisho lipi? Ukipata majibu hayo huo ndio utakuwa mwanzo wa kujua biashara gani italipa eneo hilo na hatimaye kupata faida.
Hivyo niseme hivi, biashara inayolipa na kutoa faida kubwa ni ile biashara ambayo umeshaifanyia uchunguzi wa kutosha na kujua soko lake liko wapi na lina ukubwa gani. Hiyo ndiyo biashara inayolipa.
No comments:
Post a Comment