MABASI manne ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yamechunwa na vyombo vingine vya usafiri.
Hali hiyo imetokea kutokana na kutoheshimu taratibu kunakofanywa na madereva wa vyombo vingine vya usafiri katika kipindi hiki ambacho mabasi hayo yapo kwenye mazoezi.
Hali hiyo imetokea zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa kipindi cha mpito cha mradi huo, kitakachoanza Mei 10 mwaka huu chini ya Kampuni ya Uda Rapid Transit (UDA-RT). Msemaji wa Kampuni ya UDART, Sabri Mabruki alisema,
“Sheria za mabasi haya ni kama treni, yule aliyegongwa au kagonga basi ndiye mwenye kosa”. Alitaka vyombo vya usafiri kutotumia njia maalumu za mabasi hayo na kusisitiza wananchi kuheshimu njia hizo isaidie kuepuka ajali na kurahisisha uendeshaji wa mradi.
Alisema pamoja na kupigwa marufuku madereva kupitisha vyombo vya usafiri kwenye njia za mabasi hayo, bado kuna baadhi wanapita katika barabara hizo huku mabasi yakiwa yanafanya mazoezi.
Alisema miundombinu ya mradi huo imejengwa kulingana na mahitaji, hivyo kila chombo cha usafiri kipite na waenda kwa miguu wapite katika njia zilizotengwa. Alisema mabasi yana madereva waliofuzu, yamekatiwa bima na nauli zinatarajiwa kutangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).
Alisema katika kudhibiti ulinzi wa vituo na mabasi, wamefunga kamera kwa ajili ya kubaini watu wenye nia mbaya ya kuhujumu miundombinu hiyo.
No comments:
Post a Comment