Wednesday, May 18, 2016

FAINALI KOMBE LA 'FA' YARUDISHWA NYUMA SASA KUPIGWA MEI 25

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) limerudisha nyuma tarehe ya mechi ya fainali kati ya Yanga na Azam ambapo awali ulitakiwa kufanyika Juni 11.

    Mechi hiyo sasa inatarajiwa kufanyika wiki ijayo Mei 25. Akizungumza kwa niaba ya TFF, Afisa habari Alfred Lucas amesema kuwa mechi hiyo itafanyika Jumatano ijayo badala ya tarehe ya awali iliyokuwa imetajwa na Shirikisho hilo.

     Amesema kutokana na kumalizika kwa ligi Mei 21 na timu zitakuwa zimekaa muda mrefu zikiwa hazina mechi zozote. "Ligi kuu inamalizika Jumamosi Mei 21 na wachezaji watakaa muda mrefu bila kuwa na mechi kwahiyo tumeonelea kuwa turudishe nyuma kutoka Juni 11 mpaka Mei 25,"amesema Lucas.

    Kufuatia kurudishwa nyuma kwa mechi hiyo ambayo ndiyo inatoa muwakilishi wa Michuano ya kombe la Shirikisho Afrika, TFF imezitaka timu hizo kujiandaa kwani zitakuwa  zimemaliza mechi zao za ligi kuu. Yanga watamaliza mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Majimaji mkoani Songea huku Azam watakuwa Chamazi kuumana Mgambo JKT.

     "TFF imezitaka Yanga na Azam kujiandaa zaidi  bado watakuwa hawajavunja kambi kwani wanamaliza ligi Jumamosi ya wiki hii,"amesema Lucas.

No comments:

Post a Comment