Geita. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita imewahukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela miaka watumishi wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kosa la kughushi na kumdanganya mwajiri.
Waliohukumiwa adhabu hiyo kila mmoja ni Mhasibu wa Idara ya Afya, Frank Maganga na Mtunza Bohari, Angelina Mhando baada ya kupatikana na hatia ya kutenda makosa hayo kati ya Desemba 13, 2010 na Januari 6, 2011.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Safina Simfukwe alimhukumu Maganga kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka minne au kulipa faini ya Sh6.5 milioni.
Pia, alimhukumu Mhando kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka miwili, au kulipa faini ya Sh2 milioni kwa kosa la kughushi na miaka mingine miwili na faini ya Sh2 milioni kwa kumdanganya mwajiri, adhabu zote zinakwenda sambamba. Hata hivyo, hadi Mwananchi inaondoka mahakamani hapo washtakiwa walikuwa hawajalipa faini hizo.
Wakati huohuo, Mahakama ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, imemhukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh600,000 mgambo wa Mahakama ya Mwanzo Buseresere, Majaliwa Gwakilala baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh300, 000.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Jovith Kato baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa, mshtakiwa aliomba rushwa kutoka kwa Reuben Ndimila ili asimkamate kwa kesi ya kuruka dhamana iliyokuwa likimkabilia mahakamani.
Hakimu Kato alisema baada ya kupitia ushahidi wa Takukuru na utetezi wa mshtakiwa, Mahakama imeridhika pasi na shaka kwamba mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo, hivyo hiyo iyakuwa fundisho kwa wengine.
No comments:
Post a Comment