Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella ametoa siku tano kwa Mkurugenzi wa jiji la Mwanza kuondoa dampo la uchafu lililopo mtaa wa Makoroboi, maarufu kama ‘City park’ kutokana mlundikano wa taka hizo kutoa harufu kali na kusababisha kero kwa baadhi ya wafanyabiashara waliopo katika eneo hilo.
Mongella ametoa agizo hilo wakati akipokea Madawati thelathini yaliyotolewa na shirika la umoja wa Machinga mkoa wa Mwanza, (SHIUMA) kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli katika kumaliza uhaba wa madawati nchini, baada ya machinga hao kuguswa na kilio cha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari cha kusoma wakiwa wamekaa chini.
Pamoja na changamoto zinazowakabili wamachinga, ikiwemo uhaba wa maeneo ya kufanyia biashara, ukosefu wa mitaji na elimu ya ujasiriamali, bado wameamua kuchangia sekta ya elimu kwa kila kizimba kuchangia shilingi elfu kumi na nne kwa ajili ya kuchonga madawati hayo yatakayopelekwa katika shule ya msingi Nyashana.
Mwenyekiti wa shirika la umoja wa machinga mkoa wa Mwanza Ernest Matondo anaeleza sababu zilizopelekea shule ya msingi nyashana inayokabiliwa na upungufu wa madawati 236 kupewa kipaumbele cha kukabidhiwa madawati hayo licha ya kuwepo kwa shule nyingine za wilaya ya Nyamagana zenye upungufu wa madawati.
No comments:
Post a Comment