Thursday, June 30, 2016

ROMA KUICHANA SERIKALI YA MAGUFULI

     Msanii wa HIP HOP anaesifika kwa kuichana serekali kwa vigongo vyake vingi kila anapoona maboko yupo mbioni kuachia wimbo wake mpya unaoitwa Kaa Tayari Swali la watu wengi Ujio huu mpya wa msanii huyu ataichana serekali ya Magufuli.?

       Roma amewambia mashabiki wake wakae tayari kuupokea ujio wake mpya kwani anaweza akazungumzia kitu chochote kama sukari majipu yanayotumbuliwa au hata uteuzi wa serekali ya kutumbua majipu?

      Imezoeleka kwamba Roma ni moja kati ya wasanii machachari ambao mara zote wanapotoa nyimbo za zinatumbua majipu kwa kuzungumzia vitu ambavyo haviendi sawa serekalini,ameamua kuvunja ukimya na kuachia ngoma katika serekali hii.

Wednesday, June 29, 2016

WAANDAMANA KUPINGA KUFUNGWA KWA BARABARA

   Mwanza.

     Wakazi wa Mtaa wa Kiloleli ‘B’ katika Kata ya Ibungilo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, wamepinga kitendo cha mmoja wa wakazi wa eneo hilo kufunga barabara inayounganisha mtaa huo na Mtaa wa Kiloleni ‘A’ na Nyamanoro.

      Jana asubuhi, mamia ya wakazi hao waliandamana hadi ofisi za Serikali za mtaa huo kuomba hatua za haraka zichukuliwe kumzuia mmiliki wakitalu namba 164LL kuendelea na ujenzi wa uzio huo ili kuepusha wananchi kuchukua hatua za kuuvunja kwa nguvu.

       Wataalamu wa idira ya ardhi kutoka Manispaa ya Ilemela walio ongozwa na Mpima Ardhi wa Manisapaa hiyo, Malulu Magele walilazimika kufika eneo la tukio na kuahidi kulishughulikia suala hilo ndani ya siku saba huku wakiwaasa wananchi kuwa watulivu wakati suala hilo linashughulikiwa kisheria.

       “Naomba tuwe watulivu na tuepuke kuchukua sheria mkononi kuepuka madhara wakati Serikali inashughulikia suala hili kisheria kwa faida na haki ya pande zote mbili,” amesema Malulu alipozungumza na wananchi.

MAJI YAOZESHA MBEGU ZA PAMBA

    Kahama. Tabia ya baadhi ya wakulima kuweka maji kwenye pamba kwa lengo la kuongeza uzito wakati wa kuuza imedaiwa kuwa chanzo cha upatikanaji wa mbegu zisizoota.

       Hayo yamesemwa na Meneja wa Bodi ya Pamba Tanzania Kanda ya Ziwa na Magharibi, Buluma Kalidushi alipokuwa akijibu malalamiko ya wakulima wa pamba wilayani Kahama kuhusu mbegu zisizoota wanazosambaziwa na mawakala.

       Kalidushi amesema swala la mbegu kutoota ni la wakulima wenyewe ambao huweka maji wakati wa kuuza pamba hali ambayo husababisha mbegu hizo kuoza na kampuni zinazouza mbegu hizo

      zinaponunua pamba iliyowekwa maji bila kujua kama imeoza, husambazwa kwa wakulima na kazi ya bodi ni kuhakikisha mbegu inafika vijijini kwa wakati.

      “Lakini kampuni za kuuza mbegu nazo pia zinachangia uharibifu huo kwa asilimia 50 kwa sababu zinapaswa kukagua kwanza mbegu kabla haijazinunua na kwenda kuzitolea manyoya kwa ajili ya kupandwa,” amesema Kalidushi.

ULIMWENGU AIPA MATUMAINI YANGA ITAFIKA MBALI

   Ulimwengu raia wa Tanzania amesema kwa namna Yanga wanavyocheza wanaonekana wamejiandaa kikamilifu japo kuwa kukosekana kwa uzoefu wa mashindano wa kimataifa kwa wachezaji wake ndiko kunakopelekea kushindwa kupata matokeo.

    
      Nyota huyo amekiri kukutana na wakati mgumu sana katika mchezo wa jana lakini wakaonesha nini thamani ya wachezaji wa kulipwa jambo lililowapa ushindi wa bao moja kwa sifuri wakiwa ugenini.
   
     
    Mazembe imekamata usukani wa kundi A ikiwa imejikusanyia alama sita kwenye michezo miwili ya awali huku Yanga ikiendelea kushikilia nafasi ya mwisho katika kundi lake.

NDOVU WAVAMIA MASHAMBA YA WATU UGANDA

    Ndovu kutoka mbuga ya Nimule nchini Sudan Kusini wamekuwa wakivuka na kuingia Kaskazini mwa Uganda na kuharibu mashamba ya mahindi , mihogo , viazi na pamba Maurice Vuzi ambaye ni mwenyekiti wa wa kaunti ndogo ya Dufile, alisema kuwa ndovu hao waliharibu zaidi ya ekari 35 ya mimie siku ya Jumatatu.

    Wakulima wanasema kuwa hawajui hatma yao kwa sababu kila ifikapo msimu wa kuvuna, ndovu uharibu mazao yao na wakati huu ndovu wanafika wakiwa wenge.

       Mkulima moja aliliambia gazeti la Daily Monitor kuwa hili limesababisha kushuhudiwa uhaba wa chakula katika vvjiji vilivyo eneo hilo.

UINGEREZA YAZUIWA KUHUDHURIA MKUTANO WA 'EU'

    Muungano wa Ulaya Uingereza imezuia kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Ulaya ambapo itakuwa mara ya kwanza kufanyiwa hivyo kwa miaka 40.

      Waziri Mkuu, David Cameron, hatakuwa mezani wakati viongozi wengine 27 wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Ulaya watakuwa wakihudhuria mkutano usio rasmi juu ya hatma ya muungano huo baada ya kuondoka kwa Uingereza.

  
     Uingereza imeambiwa ianzishe mpango wake wa kuondoka katika jumuiya hiyo bila kuchelewa.

  Rais wa Jumuiya ya Ulaya, Jean-Claude Junker, amesema kuwa shughuli za kutegua kujiondoa kwa Uingereza kutoka muungano huo zinapaswa kutekelezwa mara tu Uingereza inapompata Waziri Mkuu mpya.

FISI WAUWA NA KULA MTU NAIROBI

     Fisi wanakisiwa kumuua mwananme mmoja na kisha kula sehemu kubwa ya mwili wake nchini Kenya , kwa mujibu wa chifu wa eno hilo. Hii ndiyo mara ya pili kisa kama hicho kimeripotiwa katika eneo la Ongata Rongai.

       Shambulizi hilo lilitokea siku ya Jumatatu usiku, wakati mwanamme huyo alikuwa akielekea nyumbani mjini humo, ambao unakaribiana na mbuga ya wanyama ya Nairobi Hata hivyoi gazeti la Business Today liliripoti kuwa ni Simba waliyoila sehemu kubwa ya mtu huyo.

Monday, June 27, 2016

HUKUMU YA KESI YA DAUDI MWANGOSI

      Mahakamu Kuu Kanda ya Iringa imetaja siku ya tarehe 21 mwezi wa 7 mwaka huu kuwa ndio siku ya kutoa hukumu ya kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel TEN ,Daudi Mwangosi inayomkabili askari wa jeshi la polisi kikosi cha kuzuia ghasia FFU Pasificus Cleophace Simon.

       Akitoa majumuisho ya kesi hiyo Jaji wa mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Paul Kiwhelo amesema majumuisho yaliyotolewa leo ni moja ya matakwa sheria ili kuwa na mazingira bora ya kupata picha halisi ya shauri hilo la mauaji namba 25 la mwaka 2013.

      Jaji kihwelo ameieleza mahakama kuwa mnamo tarehe 2 sept 2012 mtuhumiwa Pasicuos Simon alitenda kosa hilo la mauaji na endapo mtuhumiwa akithibitika kutenda kosa hilo kwa makusudi mtuhumiwa atakabiliwa na adhabu ya kifo.

     Ameeleza kuwa jukumu la kuthibitisha kosa ni la upande wa mashtaka na linapaswa kufanyika pasipo kuacha chembe ya mashaka kwa kuzingatia ukubwa wa shauri lenyewe.

      Wakitoa majumuisho ya mwisho mahakamani hapo baada ya kusikiliza majumuisho ya upande wa jamhuri na utetezi waungwana wa mahakama wamesema mtuhumiwa alitenda kosa la mauji bila ya kukusudia. Shauri hilo la mauaji namba 25 la 2013 limepangwa kusikilizwa tena ktk hatua ya hukumu mnamo tarehe 21 mwezi wa saba mwaka huu.

MKAZI WA KIGOMA AJINYONGA KWA KINACHOSADIKIWA WIVU WA MAPENZI

    Mtu mmoja ajulikanaye kwa jina la Norbert Gidion (30) mkaazi wa Masanga katika Manispaa ya Kigoma Ujiji  amekutwa  amefariki  dunia akiwa amejinyonga kwenye mti wa mwembe kwa kile kinachosadikika kuwa ni  wivu wa mapenzi Kamanda wa polisi mkoani kigoma Afande Ferdinand Mtui,

     amethibitisha tukio hilo na kusemw kwamba upelelezi wa awali unaonesha kuwa  chanzo cha kifo cha Marehemu Norbert Gidion  ni  kutokuwepo na maelewano dhidi ya marehemu  na mke wake, Bi.Happyfania Caristus.

      "Natoa  wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa mazingira kama hayo husababisha kutokea vifo visivyotarajiwa kwa jamii:, alisema Kamanda Mtui.

     Wakielezea tukio hilo wapangaji wenzie marehemu wamesema kuwa kwa kipindi kirefu marehemu alikuwa safari hadi umauti unamkuta na kwamba  hata alivyorudi safari alikuwa halali nyumbani kwa mke wake.

     Mzazi wa marehemu Bw. Gidioni Hungu amesema  kuwa mazingira ya kifo hicho imekuwa sintofahamu kwani alikuwa hana maelewano mazuri na mkewe.

MAANDALIZI YA MAHAKAMA YA UFISADI YAANZA

    Wakati Bunge likiwa limepitisha sheria ya uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi nchini, Jukwaa la Haki Jinai ambalo linajumuisha Taasisi za umma na serikali limekutana kujipanga namna zitakavyoweza kufanya kazi kwa ufanisi kwenye Mahakama hiyo.

    Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, mara baada ya kufungua kikao hicho cha kazi cha siku mbili cha jukwaa hilo.

     Dk. Mwakyembe amesema jukwaa hilo limehudhuriwa na viongozi wote wa Taasisi ambazo zipo kwenye mfumo wa haki jinai ikiwemo Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Mahakama, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(Takukuru).

     Amesema kikao hicho kinafanyika kipindi muafaka kwa sababu leo hii tunatarajia Bunge kupitisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ambao unatoa mwanya wa kuanzisha mahakama ya mafisadi na makosa ya rushwa.

   
       Amebainisha vyombo hivyo vinaangalia jinsi gani kimoja kimoja kwa ushirikiano vitakavyoweza kufanikisha uanzishaji wa Mahakama hiyo.

      Kikao hicho kimehudhuriwa na idara ya polisi ambayo inatakiwa ipeleleze haraka, Takukuru ifanye uchunguzi kwa haraka, Timu ya DPP na waendesha mashtaka wake wote ifanye kazi kwa ufanisi sana kesi zisikae, Mahakama nayo kama kuna vitu vinakwamisha vitatuliwe. Alisema chombo hicho kinatafakari namna vyombo hivyo vitakavyoshirikiana ili mahakama hiyo iweze kufanya kazi kwa ufanisi kama Rais alivyoahidi.

       Hata hivyo alisema pamoja na hilo wanajadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika usimamiaji wa haki jinai nchini.

       Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini,Buswalo Mganga amesema changamoto zinazoikabili haki jinai nchini ni uhalifu ambao unafanywa na watanzania wenyewe na miongoni mwao wengine wanatoka nje na washirikiana na watanzania na vyombo vya habari.

"NA MIMI NATAFUTA KIKI NITOKE" KALA JEREMIAH

   Msanii kala Jeremiah amesema kitendo cha wasanii kuendeleza kiki ili waweze kuzungumziwa kwenye media kuliko kazi zao, kinaua soko la muziki na kuwaharibia kwa mashabiki.

       Akiongea kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Kala amesema imefikia hatua sasa wamewabilisha mashabiki, na kufuatilia zaidi skendo zao na sio kazi zao. "Lakini niwe mkweli suala la kiki linaharibu muziki, kwa sababu mwisho wa siku watu hawaangalii tena vipaji, mashabiki tumewabadilisha akili hawashabikii tena muziki, hawashabikii tena kipaji", alisema Kala Jeremiah.

     Pia Kala Jeremiah amesema kulingana na hali hiyo, hata yeye anafikiria kutafuta kiki kabla ya kuachia kazi yake mpya.

      "Kweli habari za kiki naziona sana nazisikia, mi mwenyewe nawaza kichwani nipige na demu gani wa bongo movie, tupige pige makiki mawili matatu alafu nitoe goma", alisema Kala.

    Kala aliendelea kusema kuwa kitndo hicho kimeharibu mpaka wasanii wachanga, ambao nao hufikiria kutoka na kiki, ili wajulikane.

    "Inahamasisha vijana hasa wasanii wachanga, ambao ndio kwanza wametoka, wanaona kama makaka zetu wanafanya hivi kwa nini na mimi nisifanye hivi ili nitoboe, lazima nitoke na kiki, lazima nitoke na kitu fulani ili niongelewe".

Sunday, June 26, 2016

WABUNGE WAPEWA SEMINA JUU YA UANZISHWAJI WA MASOKO YA BIDHAA

    Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Bibi Nasama Massinda akiwasilisha mada leo Mjini Dodoma kwa Wabunge  wa Kamati ya Bunge ya Biashara, Viwanda na Mazingira na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji( hawapo pichani)kuhusu uanzishwaji wa Masoko ya Bidhaa hapa nchini ili kuwainua wakulima.

     Kilimo kinachangia asilimia 26 ya pato la Taifa na kuchangia zaidi ya asilimia 75 ya kipato kwa wananchi waishio vijijijini, pamoja na mchango mkubwa wa kilimo kwenye uchumi wa nchi, wakulima wamekuwa wakipata matatizo mbalimbali ya masoko yenye bei zenye ushindani.

     Kwa kuliona hilo Serikali ilipitisha sera ya masoko ya bidhaa mwaka 2014 kwa kuanza na mazao manne ya majaribio ambayo ni, Korosho, Ufuta, Alizeti na Mchele.

     Hayo yamesemwa leo, mjini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Bibi. Nasama Massinda wakati wa semina  kwa Wabunge juu ya uanzishwaji wa masoko ya bidhaa nchini iliyoandaliwa na mamlaka hiyo.

        Akieleza kazi kuu za soko la bidhaa Massinda amesema kuwa soko la bidhaa linaleta uwazi wa bei za mazao na mwenendo wa soko, kila mtu ataweza kujua bei ya mazao sokoni ambapo bei zitatolewa kwa vyombo vya habari pamoja na kuondoa ulazima wa wakulima kusafirisha mazao yao toka eneo moja kwenda lingine kutafuta wanunuzi.

     “Vile vile soko la bidhaa litasaidia kutoa bei zenye ushindani kwa kuzingatia upatikanaji wa bidhaa na mahitaji ya bidhaa, litaboresha bei ya mazao vijijini kwa kuwa na soko la bidhaa litakalo toa taarifa kwa wakulima wote kuhusu soko, bei na mwenendo wa soko,” alifafanua Massinda.

      Kwa upande wake Mbunge wa Nanyamba, Mhe. Abdallah Chikota alilitaka soko hilo kupanua wigo wa uelimishaji kwa kushuka mpaka kwa wakulima na watendaji wa Serikali katika ngazi ya chini kuliko kuishia kwa mawakala ambao wanaweza wasitoe elimu hiyo kama ilivyotarajiwa.

      Soko hilo la Bidhaa linalotarajia kuanza Septemba mwaka huu linategemea kumnufaisha mkulima mdogo, wakulima wakubwa, wenye viwanda, wakusanya mazao (ushirika), wauzaji mazao nje, wakopeshaji na vyombo vya fedha pamoja na Serikali kupata mapato kupitia tozo kutokana na uwepo wa takwimu na uwazi.

KILICHOMWANGUSHA DIAMOND 'BET' 2016 HIKI HAPA

   Ni masikitiko yangu makubwa kuikosa Tuzo hii ya kimataifa kupitia msanii wetu pekee na Brand ya Afrika mashariki.

      Bila kupoteza muda Na hizi ni sababu zilimfanya Chibu Dangote

1) Hakuwa na kazi inayoeleweka ambayo ingemfanya aongeleke au jina lake lizunguke vichwani mwa watu

    2) Kumanage wasanii kwake limekua pigo kubwa maana imemfanya aache kusonga mbele akiamini amefika na ni muda wa kusaidia wengine.

     3) Kukosa baraka za mzazi mwenzake mama Tiffah kutokana na usaliti aliomfanyia mwenzake.

    4) Kurise up kwa Alikiba.

    5) Kuridhika na mafanikio Hivyo Chibu ajipange upya upya ili arudi kwenye mstari.

Saturday, June 25, 2016

BLACK COFFEE ASHINDA TUZO ILIYOWANIWA NA DIAMOND

   Los Angeles, Marekani. Mwanamuziki kutoka Afrika Kusini, Black Coffee ameshinda tuzo ya BET na kuwapiku mastaa wengine saba walioteuliwa kuwania tuzo hiyo moja tu Afrika akiwamo, Diamond Platnumz kutoka Tanzania.

    Diamond aliteuliwa kushiriki katika kipengere cha ‘Best International Act Afrika 2016’ kwa mara ya pili, baada ya kushiriki mwaka mmoja uliopita ambapo tuzo ilikwenda kwa Davido kutoka Nigeria.

      Diamond alikuwa akichuana na baadhi ya mastaa wa Afrika akiwamo Yemi Alade, Wizkid kutoka Nigeria, maarufu ‘Black Coffee’ na Cassper Nyovest  wote kutoka Afrika Kusini, huku wengine wakiwa ni Mzvee (Ghana) na Serge Beynaud (Cote D’ivoire).

      Hata hivyo, Diamond atafanya shoo katika jukwaa hilo na itakuwa ni shoo ya kwanza kwake tangu kuanza kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo baada ya shoo hiyo, ametangaza ratiba ya shoo zake zingine zinazofuatia.

     Hii ni mara ya pili kwa Diamond kuteuliwa kuwania tuzo hiyo kubwa duniani.

WANAFUNZI 24500 WAKOSA SHULE NCHINI

   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene  Dodoma.

     Jumla ya wanafunzi 24,528 ambao ni zaidi ya robo ya wenye sifa ya kujiunga na kidato cha tano wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato hicho na shule za ufundi kutokana na uhaba wa shule. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alitoa takwimu hizo jana akibainisha kuwa hata hivyo, ufaulu kwa wanafunzi hao kwa mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka jana.

      Simbachwene alisema majaliwa ya wanafunzi waliokosa shule, ni kusubiri uchaguzi wa pili baada ya muda wa kuripoti kuwadia na kusiwe na wanafunzi waliochaguliwa lakini hawakuripoti kwenye shule za Serikali.

       Kati ya waliokosa nafasi hizo, wasichana ni 6,789 na wavulana 17,739 na 348 ambao wameachwa kwa sababu umri wao umezidi miaka 24 inayotakiwa. Wanafunzi 625 wamekosa sifa kutokana na ufaulu wao kutokuwa na masomo ya mlingano (tahasusi).

       Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, wanafunzi 393,734 walifanya mtihani na kati yao 90,380 (wasichana 36,005 na wavulana 54,375) walifaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu na hao ndiyo walioshindanishwa kujiunga na kidato cha tano,” alisema Simbachawene.

       Alisema wanafunzi hao watapangwa katika shule 326 zikiwamo mpya 47 na muhula wa masomo unatarajia kuanza Julai 11 na wanatakiwa kuwa wameripoti shuleni si zaidi ya Julai 25. Simbachawene alisema asilimia 52 ya wanafunzi waliochaguliwa ambao ni 34,064 watajiunga kwa masomo ya sayansi wakiwamo wavulana 20,598 na wasichana 13,466.

      “Kwa masomo ya Sanaa na Biashara wamechaguliwa wanafunzi 30,897, kati yao wasichana ni 15,445 na wavulana 15,452. Wanafunzi wanaokwenda vyuo vya ufundi ni 759 kati yao wasichana wakiwa 220 na wavulana 539.

Thursday, June 23, 2016

AZAM KUANZA KUJIFUA JULAI MOSI

     BAADA ya mapumziko ya takribani mwezi mmoja kwa kumalizika msimu uliopita, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imebakiza siku nane tu kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa 2016-17.

        Wachezaji wote wa Azam FC wanatarajia kurejea klabuni  Juni 29 mwaka huu kuanza maandalizi hayo na wataanza rasmi mazoezi Julai Mosi mwaka huu katika makao makuu ya klabu Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Makocha wapya wa Azam FC kutoka nchini Hispania, nao watatua nchini wiki ijayo wakiongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez,

   
      Kocha wa Viungo Jonas Garcia, watakaokuja na wataalamu wengine wa ufundi watatu, Kocha Msaidizi atayekuwa sambamba na Msaidizi wa sasa Dennis Kitambi, wa Makipa na Daktari wa timu. Kazi ya kwanza ya makocha hao mara baada ya kuwasili itakuwa ni kushughulikia zoezi la usajili linaloendelea hivi sasa,

  
     ambapo watatoa hatima y wachezaji wanaobakia ndani ya timu na watakaoachwa pamoja na kuongeza nguvu mpya kwa ajili ya kukipa makali kikosi hicho msimu ujao. Mabingwa hao wataanza msimu kwa kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) wakiwa kama mabingwa watetezi baada ya mwaka jana kuutwaa ubingwa huo kwa rekodi ya aina yake ya kutofungwa mchezo wowote wala kuruhusu bao ndani ya dakika 90.

        Michuano hiyo inatarajia kuanza katikati ya mwezi ujao, ambapo Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) liko kwenye hatua za mwisho za kuitangaza nchi itayoandaa baada ya Tanzania kujitoa. Azam FC pia itakuwa ikijiandaa vilivyo kupigania mataji ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu ujao na ubingwa wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation pamoja na kutimiza adhma yake ya kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

      Ikumbukwe kuwa mbali na Azam FC kutwaa ubingwa wa Kagame Cup msimu uliopita, pia ilifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye ligi na FA Cup huku pia ikiishia hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.  

ZITTO AMCHACHAMALIA MAGUFULI

    ZITTO Kabwe, kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo ametoa tamko lake juu ya kauli ya Rais John Magufuli ya kupiga marufuku vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa zaidi ya bungeni na kwenye kampeni za mwaka 2020 ni sawa na kuua demokrasia.

     Tumepokea kwa MSHTUKO na masikitiko makubwa kauli ya Rais kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya siasa isipokuwa wakati wa kampeni na kupitia bungeni.

       Tunaichukulia kauli ya Rais kama tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini. Chama chetu kitaitisha vikao vya dharura kujadili hali ya nchi na namna ya kukabiliana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya demokrasia nchini mwetu. Tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa nchini kuunganisha nguvu katika kuhakikisha tunapigana vita hii pamoja.

        Huu ni wakati wa vyama vya siasa na wanasiasa kuacha tofauti zao na kupambana kulinda uhuru wa kufanya siasa wakati wowote kwa mujibu wa Sheria. Tunatoa wito kwa wananchi wote na taasisi za kiraia kusimama imara katika kulinda demokrasia.


       Tunasisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa huwezi kuua demokrasia bila kuua juhudi za maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote mwenye mamlaka kuua demokrasia nchini mwetu. Hatua zozote za kuua demokrasia ni kuua Umoja, Amani na mshikamano wa wananchi na Taifa, ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yetu kijamii, kisiasa na kiuchumi.

        Tunatoa wito kwa wananchi wote kushikamana na kusimama imara katika kulinda demokrasia. Zitto Kabwe, MB Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo

SANGOMA WAPANDISHWA KORTINI

    WATU watatu wanaosadikika kuwa waganga wa kienyeji wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa la kosa utapeli Akisoma mashtka hayo Nassoro Katuga,

     mbele ya Magreth Bankika, Hakimu Mkazi katika mahakama hiyo amesema, kwa waakati tofauti mwaka 2012 katika eneo lisilojulikana kwa pamoja walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.


      Katuga amedai kuwa, kati ya mwezi Januari hadi Desemba 2012 eneo la Kibamba, Kinondoni jijini Dar es Salaam walidanganya na kijipatia kiasi cha Sh. 260 milioni kutoka kwa Sophia Lolila kwa kujifanya waganga na kudai watamsaidia kwa nguvu za giza aolewe, kupata watoto na biashara yake ya mbao itaenda vizuri.

       Katuga amesema kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba, kesi hiyo itajwe kwa usikilizwaji wa awali. Washtakiwa wote wamekana mashitaka hayo.

     Dhamana ya washitakiwa ipo wazi kwa mashrti ya kila mmoja awe na wadhamini wawili na kusaini hati ya dhamana ya Sh. 43.3Milioni kila mmoja.Kesi itatajwa tena Julai 4 Mwaka huu.

IBRAHIMOVIC ASTAAFU RASMI SOKA LA KIMATAIFA

   Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic amestaafu rasmi kuitumikia timu yake ya taifa ya Sweden ambapo jana timu yake iliondolewa kwenye michuano ya Euro 2016 baada ya kufungwa 1-0 na Ubelgiji na huo kuwa mchezo wake wa mwisho.

       Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34, siku ya Jumanne wiki hii, alitangaza kuwa michuano ya Euro 2016 itakuwa michuano yake ya mwisho kuitumikia timu yake ya taifa. Alifunga mabao 62 katika michezo 116, lakini alishindwa kutikisa wavu katika Euro mwaka huu.

        Aidha, Ibrahimovic hataiwakilisha tena nchi yake katika Rio Olimpiki kama ilivyokuwa imefikiriwa hapo awali. Kocha wa Sweden, Erik Hamren amesema, "Katika nchi ndogo kama Sweden, huwezi kupata mchezaji mwingine kama yeye, kweli yeye ni wa kipekee."

        Sweden haikufanikiwa kuishinda timu yoyote kwenye kundi E, katika mechi yake na Ireland ilitoka sare ya 1-1 na kupoteza michezo yote ya Italia na Ubelgiji.

     Mshambuliaji huyo wa zamani wa Ajax, Barcelona, Juventus na Inter Milan amekuwa akihusishwa kuhamia Manchester United tangu kuamua kuondoka Paris St-Germain.

WANAUME AMBAO WATAFANYA UASHERATI WATAFUNGWA CAMEROON

   Wanaume ambao hushiriki uasherati watafungwa jela, chini ya sheria mpya ambayo inajadiliwa na bunge la Cameroon. Mswada huo ambao ulipata uungwaji mkono wa chama cha Rais Paul Biya, unatarajiwa kuidhinishwa.

      Kwa sasa wanawake wanaweza kufungwa jela kwa kati ya miezi miwili na sita kwa kufanya mapenzi nje ya ndoa. Wakosoaji wanasema kuwa sheria hiyo itairudisha nyuma Cameroon, na kusababisha watu wengi kufungwa.

MTOTO ANAJISIWA NA KISHA KUUAWA KWA KUNYONGWA

   Eneo la Unga Limited, jijini Arusha Mtoto wa miaka minne amenajisiwa na kuvunjwa shingo na kutupwa kandokando ya njia ya watembea kwa miguu karibu na mfereji wa maji umbali wa mita 50 kutoka nyumbani kwao jijini Arusha.

       Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuf Ilembo, tukio la kunajisiwa kwa mtoto huyo wa kike lilitokea Juni 20, mwaka huu saa 3.30 usiku kwenye makaburi ya baniani Kata ya Unga Limited.

     Kaimu Kamanda wa Polisi Ilembo alidai mtoto huyo ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa akicheza na wenzake nje kidogo ya nyumbani kwao na ilipofika saa 12 jioni kwa mujibu wa marafiki zake (majina yamehifadhiwa) wanasema alifika mtu mmoja mwanamume mrefu.

      Kwa mujibu wa watoto hao, mwanamume huyo alikuwa amevaa suruali na kumwambia mtoto huyo amfuate akamnunulie pipi na hapo ndipo alipomfuata huyo mwanamume huyo na hakurudi tena.

ARGENTINA VS CHILE NI FAINALI YA MARUDIO YA 2015

     Chile imeifunga Colombia kwa bao 2-0 kwenye mchezo wa nusu fainali ya Copa America Centenario na itakutana na Argentina kwenye mchezo wa fainali kwenye uwanja wa MetLife mchezo wa fainali unaozikutanisha timu hizo baada ya mwaka mmoja.


       Magoli ya mapema ya Charles Aranguiz na Jose Fuenzalida yaliipa La Roja  uongozi wa game hiyo mapema , licha ya Colombia kutengeneza nafasi za kutosha, hawakuweza kubadili matokeo hayo.

       Chile na Argentina zimekuwa ni bora kwenye mashindano kwa muda mrefu na zinastahili kupambana kuwania ndoo ya Copa America kwenye mchezo wa fainali siku ya Jumapili. Ni nafasi kwa Argentina kulipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya michuano hiyo mbele ya Chile waliokuwa wenyeji wa mashindano mwaka uliopita.

     Chile watakuwa na faida ya urejeo wa kiungo wao Vidal huku Diaz akitarajiwa kuwepo kwenye kikosi baada ya kuwa majeruhi huku kikosi kizima kikiwa kwenye form nzuri. Argentina ndiyo wanapewa nafasi kubwa kwasababu ya walishaichapa Chile bao 2-1 kwenye hatua ya makundi.

       Argentina walicheza mchezo huo bila ya uwepo wa nyota wao Lionel Messi aliyekuwa akiuguza maumivu ya mbavu. Wakiwa bila ya Ezequiel Lavezzi ambaye anauguza majeraha ya kiwiko, kikosi cha Tata Martino bado kina nyota wengine wengi ambao wanaweza kuziba nafasi hiyo.

      Argentina watakuwa kwenye presha kubwa ukilinganisha na Chile. La Albiceleste  haijafanikiwa kutwaa taji hilo tangu ilipolinyakua kwa mara ya mwisho mwaka 1993. Baada ya kupoteza fainali mbili hivi karibuni ile ya Kombe la Dunia pamoja na Copa America, watakuwa wanataka kurekebisha makosa.

       Messi bado ameendelea kukumbwa na jinamizi la kushindwa kutwaa mataji akiwa na timu yake ya taifa, Jumapili itakuwa ni nafasi yake nyingine ya kukamilisha ndoto zake za muda mrefu.

UGONJWA ULIOZUIA MAHAFALI YA CHADEMA WAJULIKANA

  Dodoma.

     Serikali imesema uchunguzi wa awali wa vifo vya watu wanane mkoani Dodoma umeonyesha kuwa vilitokana na familia kula ugali wa unga wa mahindi wenye sumu kuvu B (aflatoxins B). Jeshi la Polisi lilizuia mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya mkoani Dodoma ambao ni wafuasi wa Chadema yaliyokuwa yafanyike kwenye hoteli ya African Dream,

     likisema mikusanyiko yote imezuiwa baada ya kuzuka ugonjwa usiojulikana ambao awali uliua watu sita. Wakati Jeshi la Polisi likizuia mahafali hayo ya Chadema, taasisi nyingine zilikuwa zikiendelea na mikutano kwenye hoteli hiyo, jambo lililowafanya viongozi wa Chadema kulalamikia hafla yao kusambaratishwa na polisi waliokuwa na silaha za moto na gari la maji ya washawasha.

     Mbali na kuongezeka kwa idadi ya waliofariki dunia, watu waliougua ugonjwa huo wameongezeka kutoka 21 hadi 28. Naibu Waziri wa Afya, Dk Khamis Kigwangalla alisema pamoja na matokeo hayo ya awali, watalaamu wengine wa afya walienda wilaya za Chemba na Kondoa kuchukua sampuli nyingine.

      Alisema wataalamu hao wanatoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). Alisema sumu kuvu inatokana na fangasi wanaokuwa katika mazao ya nafaka au mahali ambapo mazao hayo yamehifadhiwa.

        Hata hivyo, alisema athari za sumu kuvu hizo ni za muda mrefu na inamuweka mtu katika hatari ya kupata saratani ya ini. Dk Kigwangalah alisema uchunguzi huo umethibitisha kuwa ugonjwa huo si Homa ya Bonde la Ufa wala manjano, ingawa baadhi ya dalili zinafanana. Jumapili iliyopita Waziri wa Afya,

      Ummy Mwalimu, alisema wamechukua hatua mbalimbali ikiwamo kuchukua sampuli za maabara kwa ajili ya utambuzi wa ugonjwa na damu, mkojo, kinyesi, matapishi na vinyama vinavyotokana na ini vimechukuliwa.

     “Sampuli zote zimepelekwa Maabara ya Taifa, Mkemia Mkuu wa Serikali na Maabara ya Kilimanjaro Christian Research Institute (KCRI) iliyopo Kilimanjaro kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

USIPODAI RISITI JELA MIAKA MITATU

     Dodoma. Mtu atakayeshindwa kutoa au kudai risiti anakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyopungua Sh3 milioni, iwapo muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 utapitishwa na Bunge.

       Kuwasilishwa kwa muswada huo ni mwendelezo wa agizo la Rais John Magufuli la kuwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kudai risiti kwa malipo wanayoyafanya, kwa kuwa ndani yake kuna ‘percentage’ ya Serikali kwa masuala ya maendeleo. Muswada uliowasilishwa bungeni awali Juni 8, kifungu cha 61 kinapendekeza kufanyia marekebisho kifungu cha 86 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015 na kuongeza makosa katika matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD).

      Moja ya mapendekezo ya makosa hayo ni mtu kutodai risiti au kushindwa kuripoti kuwa amenyimwa risiti, au ankara ya malipo wakati wa kununua bidhaa na huduma. Awali kifungu hicho kilikuwa kikijumuisha kosa moja tu la mfanyabiashara kutotumia EFD au kutotoa risiti au kutotoa ankara ya malipo na adhabu, ilikuwa faini isiyopungua Sh1.5 milioni au kuzidi Sh 2.25 milioni au kifungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

        Adhabu iliyopendekezwa katika makosa hayo iwapo mtu atatiwa hatiani ni faini ya kiasi kisichopungua Sh3 milioni na kisichozidi Sh4.5 milioni au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja. Iwapo hakutakuwa na mabadiliko makubwa yatakayowasilishwa leo,

     muswada huo ulikuwa unapendekeza kuwa mbali na adhabu hiyo, atakayekutwa na makosa hayo pia atatakiwa kulipa faini mara mbili ya kodi aliyokwepa au kifungo kisichopungua miaka mitatu. Hata hivyo, taarifa kutoka ndani zinaeleza kuwa kamati inapendekeza adhabu hiyo ipunguzwe angalau faini iwe isiyozidi Sh 30,000 na kifungo kisichozidi miezi sita.

       Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia alisema iwapo kuna jambo hilo itajulikana leo bungeni atakaposoma mapendekezo ya kamati yake. Muswada huo utawasilishwa leo kwa mara pili na kujadiliwa na wabunge kabla ya kuupitisha baada ya kuahirishwa mara mbili kutokana na Kamati ya Bajeti kutokamilisha kazi yake kwa wakati.

       Awali zilikuwepo taarifa kuwa kulikuwa na mvutano kati ya kamati na baadhi ya wabunge waliotaka mapendekezo yao yazingatiwe yakiwamo ya kupinga kuanzishwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye huduma za utalii na kodi ya usajili wa bodaboda.

       Lakini jana, Ghasia alieleza kuwa hakukuwa na mvutano wowote na kwamba wabunge wenye mapendekezo ya majedwali ya marekebisho walishauriwa kuyawasilisha bungeni. Alisema sababu ya kuchelewesha muswada huo ni ufinyu wa muda wa kamati kukutana na Waziri wa Fedha na Mipango na pia wajumbe kuchambua kwa kina masuala yaliyomo kutokana na kuwepo mapendekezo ya maboresho ya sheria nyingi.

     “Tofauti na miaka ya nyuma, bajeti imesomwa Jumatano, tulipumzika Alhamisi na siku zote hizo waziri alikuwa bungeni alikosa nafasi ya kukaa na alianza kukaa na kamati Ijumaa iliyopita hivyo muda ulitubana.

      “Ila tumeshamaliza tangu jana saa nane usiku na tunahitaji taarifa iandikwe na kusahihishwa hivyo tuliomba Serikali itusubiri na kesho (leo) muswada utaingia bungeni,” alisema. Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa tarehe ya mwisho ya muswada huo kuingia bungeni ilikuwa jana lakini kutokana na kamati kutomaliza kazi yake ilibidi wasubiri ila leo utawasilishwa na kujadiliwa.  

      Muswada huo unawasilishwa huku wabunge wengi wakionyesha kutoridhishwa na baadhi ya hatua za kikodi zilizochukuliwa na Serikali wakisema zitawaumiza wananchi.

     Mbunge wa Nzega Mjini(CCM), Hussein Bashe alieleza jana kuwa amejiandaa kumbana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwa kupeleka jedwali la marekebisho la kuondoa ongezeko la kodi  ya usajili wa magari, bodaboda na mitumba. Bashe aliwaambia wanahabari bungeni jana kuwa marekebisho hayo atayawasilisha leo.

    Alisema marekebisho mengine ni kodi katika utalii, kufuta kodi katika mazao yasiyosindikwa, uhamishaji wa fedha na Sheria ya Mawasiliano ambayo inalazimisha makampuni ya simu kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Alipinga kulazimisha kampuni za simu kujisajili katika soko hilo ndani ya miezi sita kwa sababu hiyo itaua thamani za kampuni hizo. Alisema badala yake Serikali iweke vivutio kama kupunguza kodi mbalimbali, hali itakayofanya kampuni si tu za simu bali na nyingine kujiunga na soko hilo.

        “Pia nimeishauri vyanzo vingine vya mapato ambavyo havitaathiri bajeti kuu. Wao kama watahitaji mabadiliko ya sheria nyingine kuwezesha vyanzo vipya walete kwenye mkutano wa mwezi wa tisa,”alisema.

     Alivitaja vyanzo vipya vya mapato kuwa ni pamoja na uvuvi katika bahari kuu ambapo kutakuwa na mapato ya Sh200 bilioni. “Kwa kuanzisha soko la madini, watu wawe wanaingia na madini yao bila kutozwa ushuru tutapata fedha kwa watu kulala katika hoteli, kununua vitu na tutakayotoza kwa kuuza madini nje ya nchi,”alisema.

      Hata hivyo, juzi jioni wakati Dk Mpango akizungumza na wanahabari katika mkutano wa dharura alionyesha kutupilia mbali sehemu kubwa ya mapendekezo ya wabunge yakiwamo kuondoa VAT katika huduma za utalii na kodi ya usajili katika bodaboda na magari. Alisema hata kabla ya pendekezo la VAT kwenye utalii, Tanzania bado ilikuwa na watalii wachache kuliko washindani wake kama Kenya na Afrika Kusini lakini mapato yalikuwa makubwa. “Watalii hawangalii vigezo vya kodi pekee.

         Wanaangalia hali ya usalama, miundombinu ya hoteli, barabara, hospitali bora na vivutio vizuri.” Katika hoja ya wabunge kuondoa kodi ya usajili wa bodaboda iliyopanda kutoka Sh150,000 hadi Sh 250,000, Dk Mpango alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kulipa kodi na Rais ameshaonyesha mfano kwa kubali kukatwa kodi katika kiinua mgongo chake hivyo wamiliki hao wa pikipiki hawana namna zaidi ya kuilipa kodi hiyo.

    Ni pendekezo moja tu la wabunge na wadau lilizingatiwa ambalo ni kufuta pendekezo la awali la ufutaji misamaha ya kodi kwa taasisi za dini kwa maelezo kuwa iwapo lingetekelezwa lingechelewesha utoaji wa huduma za elimu na afya kwa wananchi kupitia taasisi hizo.

Wednesday, June 22, 2016

MAGUFULI AZIGEUKIA KAMPUNI ZA SIMU

   VbRAIS John Magufuli ameagiza kwa taasisi zinazosimamia fedha na kodi, kuhakikisha kuwa serikali inakusanya kodi kwenye miamala ya fedha, inayofanywa na taasisi hizo na kampuni za simu na za madini.

        Aidha, ameagiza kuwa Sh bilioni saba zilizolipwa kwa pensheni hewa, zirejeshwe mara moja huku akitoa ufafanuzi wa hatua ya serikali ya kusitisha kwa muda ajira serikalini. Rais Magufuli alisema hayo Dar es Salaam jana katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na uzinduzi wa sarafu maalumu yenye thamani ya Sh 50,000 na vitabu viwili, kikiwemo vinavyozungumzia masuala ya fedha na uchumi.

        Uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam, ulikwenda pamoja na kongamano lililojadili mada kuhusu namna ya kupata fedha za miradi ya maendeleo zaidi ya misaada na mikopo nafuu na athari zake iliyowasilishwa na Profesa Justin Lin wa Chuo Kikuu cha Peiking, China. Rais Magufuli alisema takwimu zinaonesha katika mwezi mmoja wa Machi, miamala iliyofanywa na kampuni za simu za mkononi ni ya zaidi ya Sh trilioni 5.5, lakini alihoji ni kasi gani cha kodi kimeingia serikalini.

       Alisema pamoja na kusimamia makusanyo ya kodi za serikali, pia aliagiza BoT, Hazina na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wajipange kuhakikisha mtambo wa kudhibiti makusanyo ya kodi, unafanya kazi na kufuatilia usalama wa huduma za fedha. Mbali na hilo, aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha serikali inakusanya kodi zinazostahili kutoka kwenye kampuni za madini na kufuatilia kwa karibu, kwa kuwa kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya kampuni.

       “Unakuta kampuni ipo nchini mwaka wa kwanza hadi wa 10, wanakwambia hawapati faida lakini wanaendelea kuchimba dhahabu. Sasa eneo hilo liangaliwe kwa karibu na kama kampuni inashindwa bora iondoke, ni heri tubaki na dhahabu yetu hata miaka 1000 ijayo, watakuja kuchimba wengine wakati sisi tumeshaoza. Visingizio vya kupata hasara kila mwaka, lakini wanaendelea kuwepo, haiwezekani,” alisema. Aliwataka watendaji hao kutokuwa na kigugumizi katika kusimamia rasilimali kwa manufaa ya Taifa na kwamba serikali ina imani kubwa na BoT, hivyo wakisimamia vizuri uchumi utaimarika.


        Pensheni hewa Aidha, aliwataka viongozi wa taasisi hizo pia kushirikiana katika kudhibiti malipo kwa watumishi hewa, ambayo sasa imefikia kwenye utoaji wa pensheni hewa. Alisema anazo taarifa kuna wafanyakazi hewa 2,800, ambao wamelipwa pensheni hewa ya Sh bilioni saba kupitia Benki ya NMB, na kuagiza fedha hizo zifuatiliwe na benki hiyo izirejeshe mara moja.

     
        “Wakati nazungumzia watumishi hewa ndani ya serikali wamefikia 12,446 na kwamba inawezekana idadi hiyo ikaongezeka na sasa watumishi hao wamelipwa pensheni shilingi bilioni saba,” alisema. Rais Magufuli alisema wakati serikali inahakiki wafanyakazi hewa, Utumishi waliendelea kuajiri wapya, jambo ambalo kwa sasa amelisimamisha kwa miezi miwili ili kutoa nafasi ya kushughulikia changamoto hiyo.

        Kusitishwa ajira “Nilisema ajira mpya zisimame kwa mwezi mmoja na nusu lakini haitazidi miezi miwili, nawaomba watumishi msivunjike moyo kwa kuwa serikali imegundua kosa lazima lirekebishwe, lazima tujipange. Hata kupandisha vyeo tumesimamisha kwa muda huo baadae tutaendelea, tunataka kujenga nidhamu,” alisema. Pia aliitaka BoT kufuatilia kwa karibu utendaji wa benki na kuchukua hatua kwa benki, ambazo hazifanyi kazi vizuri hata kama zinamilikiwa na serikali. “Benki mojawapo ni Twiga Bancorp, haifanyi kazi vizuri, inajiendesha kwa hasara na serikali imekuwa ikiipatia fedha kila mwaka za uendeshaji. Hasara imefikia shilingi bilioni 18.

        Naomba Katibu Mkuu Hazina na BoT mfuatilie kama imeshindwa kujiendesha ifungwe. “Katika utawala wangu sitabembeleza, nataka watu wafanye kazi kama benki haizalishi ni afadhali ikafungwa kuliko kuendelea kuitia hasara serikali. Kuna benki nyingine nayo ambapo inapigiwa debe na wanasiasa tena wa CCM lakini nayo haifanyi vizuri,” alisema. Alisema kwa kuwa Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, sio mwanasiasa, anapaswa kufanya kazi yake bila kujali kama benki ni mali ya serikali au la, na kuwaacha wanasiasa waendelee na yao.

         Aidha, aliagiza BoT kufuatilia suala la akaunti zilizolala kwenye benki kwa kuwa wakati mwingine fedha zinakaa mpaka watu wanapanga kuzitorosha. “Najua kwenye akaunti hizo kuna fedha nyingi, kuna akaunti moja ina Sh bilioni 23. Nataka mfuatilie na mimi nafuatilia kwa karibu,” alisema. Pia aliwataka BoT kufuatilia kwa karibu maduka ya kubadilisha fedha ili wafanye biashara halali na yasitumike vibaya kutorosha fedha ama kutakatisha fedha haramu zikiwemo za wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

        Mfumuko wa bei Alisema kwamba jukumu kubwa la BoT ni kudhibiti mfumuko wa bei na katika kipindi cha miaka ya 1990 hadi mwaka huu, Benki Kuu imefanya kazi kubwa ya kupunguza mfumuko wa bei kutoka asilimia 30 hadi asilimia 5.2. Hata hivyo, alisema kupungua huko kunaonekana vizuri kwenye takwimu, lakini katika uhalisia wa maisha ya watu bado kuna changamoto kubwa; na wakati mwingine wananchi wanaona kama mfumuko wa bei umeongezeka hadi kufikia asilimia 70.

        Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza watendaji wa BoT wakiongozwa na Gavana Ndulu, kuhakikisha hiyo asilimia iliyopungua inaonekana kwenye maisha ya wananchi wa kawaida kwa maana ya bei za bidhaa kupungua. Aliwapongeza wafanyakazi wa BoT chini ya uongozi wa Profesa Ndulu kwa mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka 50, ikiwemo kuongeza benki kutoka tatu hadi 54 ambazo zimeendelea kufanya kazi na kutoa mikopo. Fedha vijijini Hata hivyo, alisema

         kuna haja ya BoT kuhakikisha huduma za fedha zinafikishwa vijijini ambako kuna zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania badala ya kubaki mijini, ambako kwa sehemu kubwa wanafanya biashara na serikali. Alisema pia taasisi za fedha zimeendelea kutoa mikopo na kutoza riba kubwa, ambapo sehemu kubwa ya wakopaji wamejikuta wakishindwa kuendelea na wengine kufilisika kutokana kulipa fedha nyingi za riba kwenye mikopo.

REAL MADRID KUMRUDISHA ALVARO MORATO

    Klabu ya ​Real Madrid imetangaza kumrudisha mshambuliaji wao wa zamani Alvaro Morata hivyo atajiunga nao kwenye msimu ujao akitokea klabu ya Juventus.

      Morata mwenye umri wa miaka 23, ambaye ni mchezaji wa Hispania anayeshirikia michuano ya Euro 2016, alijiunga na Juventus mwaka 2014, baada ya misimu minne na Real Madrid kuisha.

      Alifunga magoli 27 katika miaka miwili akiwa Juventus na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili. Mshambuliaji huyo hadia sasa ameshaifungia nchi yake magoli tatu katika michuano ya Euro 2016 inayoendelea nchini Ufaransa.

HATIMA YA LUGUMI MIKONONI MWA SPIKA

   Dodoma. Hatima ya ripoti ya Kampuni ya Lugumi inayodaiwa kushindwa kutekeleza mradi wa kufunga vifaa vya utambuzi wa vidole kwenye vituo vya polisi, ipo mikononi mwa Spika wa Bunge.

     Akizungumza bungeni jana, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo iliyoundwa kufuatilia sakata hilo, Japhet Hasunga alisema bado ripoti hiyo ipo mikononi mwao kwa ajili ya marekebisho.

      “Bado tunaifanyia marekebisho ili iendane na hadidu za rejea tulizopewa, baada ya hapo tutaipeleka kwenye kamati na wao baada ya kuridhia wataipeleka kwa Spika,” alisema. Hasunga ambaye pia ni mbunge huyo wa Vwawa (CCM), alisema uamuzi wa kama taarifa ipelekwe bungeni utakuwa wa Spika. Alisema kabla ya kumalizika kwa mkutano wa bajeti unaoendelea ripoti hiyo itakuwa tayari.

      Kamati ndogo iliundwa kutoka Kamati ya Hesabu za Serikali, (PAC) ili kuchunguza sakata hilo na kuandika ripoti kwa kamati. Mbunge huyo alisema kamati ilipewa kazi ya kuchunguza undani wa mkataba huo wenye thamani ya Sh37 bilioni Aprili 23, mwaka huu.

MZAMBIA MPYA WA YANGA APEWA JEZI YA COUTINHO

  SIKU chache baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Yanga, uongozi wa Yanga umemkabidhi jezi namba saba mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa.

   Chirwa alitua nchini wiki iliyopita akitokea FC Platinum ya Zimbabwe aliyokuwa anaichezea pamoja na mshambuliaji tegemeo, Donald Ngoma. Mzambia huyo, alisaini kuichezea Yanga akichukua nafasi ya Mniger,

    Issoufou Aboubacar aliyesitishiwa mkataba wake wa kuendelea kukipiga Jangwani hivi karibuni. Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema jezi iliyobaki ni namba saba iliyokuwa inavaliwa na Mbrazili, Andrey Coutihno.

     Saleh alisema, jezi hiyo huenda akaanza kuonekana akiivaa mechi na Mazembe itakayochezwa Jumanne  ijayo mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

    "Chirwa tumempatia jezi namba saba iliyokuwa ikivaliwa na Coutinho, jezi ambayo haina mtu kwa hivi sasa tangu ameondoka Mbrazili huyo.

     "Hivyo jezi ataanza kuonekana akiivaa kwa kuanzia mechi na Mazembe na nyingine zote zitakazofuata za michuano ya kimataifa,"alisema Saleh. Chirwa akiwa anaichezea Platinum, alikuwa anaivaa jezi namba 9 inayovaliwa hivi sasa na beki raia wa Togo, Vincent Bossou.

TAMBUA WATU WALIOTEMBELEA PROFILE YAKO YA FACEBOOK BILA YA WEWE KUJUA

    Nimekuwa nikiona watu wengi wakitumia application kutambua niwatu gani ambao wametembeleaprofile zao za facebook..sasa nimewaleteanjia moja na rahisi isiyohitaji wewe kutumia application yeyote ile..

FUATA MAELEZO HAYA

1-nenda katika profile yako ya facebook

2-binya CTRL na herufi U yani CTRL+U kisha chagua au right click mouse yako kisha chagua ” View Page Source ”

3-kisha binya CTRL na F yani CTRL+F kisha kitatokea kibox kidogo ndani ya kibox hicho andika maneno haya  ordered_list.top_friends.

    kama hivi baada ya hapo utaona profile id za watu wote kama ionekanavyokatika picha hii hizo namba ambazo ziko katika vifungo ndo profile za watu hao pasipo majina yao sasa jinsi ya kuona profile za waliotembelea na kukutizama facebook ni hivi..

   mimi nitachagua profile ambayo nimeichorea rangi ya blue ambayoni 100000617054353..

nenda kwenye adress bar. kisha type https://www.facebook.com/100000617054353 Natumai utakuwa umeipenda post hii usisahau

   kulike page yetu ilikuweza kupokea tips zingne direct kupitia facebook www.facebook.com/NyumbaYaHabari

MOISE KATUMBI AHUKUMIWA MIAKA 3 JELA

  VMgombea urais wa upinzani nchini Jamhuri ya Demokrasi ya Congo Moise Katumbi, amehukumiwa kifungo cha miaka 3 jela kwa kununua nyumba kinyume cha sheria kwenye mji ulio mashariki mwa nchi wa Lubumbashi. Pia alipigwa faini ya dola milioni 6.

     Katumbi hakuwa mahakamani wakati wa kutolewa kwa hukumu hiyo, baada ya kusafiri kwenda afrika kusini kupata matibabu siku moja baada ya serikali kutangaza waranti wa kukamatwa kwake kwa mashtaka tofauti.

      Analaumiwa kwa kuwaajiri mamluki wa kigeni ili kipanga njama dhidi ya serikali. Katumbi amekosoa hukumu hiyo, akisema kuwa ni jaribio la kutaka kuchelewesha kampeni yake ya kutaka kumrithi Rais Joseph Kabila mwezi Novemba.

WATU 2 WAUAWA KWENYE GHASIA AFRIKA KUSINI

    Watu wawili wanaripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na 40 kujeruhiwa wakati wa maandamano yenye ghasia kwenye mji mkuu wa Afrika Kusini Pretoria.

    Maandamano hayo ni ya kupinga hatua ya chama tawala nchini humo cha African National Congress (ANC) ya kumteua mgombea wa kiti cha umeya mwezi Agosti.

   Uporaji kwenye maduka yakiwemo yale yanayomilikiwa na wahamiaji, umeendelea siku nzima licha ya kuwa wa kiwango cha chini ikilinganishwa na hapo jana na Jumatatu

TANI 5 ZA KAHAWA ZAKAMATWA WILAYANI KYELA

   Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kupitia kamati yake ya mapato na kudhibiti biashara ya magendo imekamata zaidi ya tani tano za kahawa zenye thamani ya  shilingi milioni 6  zikivushwa kimagendo nje ya nchi.

   Biashara ya kahawa na maharage iliyokuwa ikifanyika katika njia zisizo rasmi na kuacha nchi ikikosa mapato yake, sasa huenda ikaanza kufuata utaratibu mara baada ya serikali katika wilaya ya Kyerwa,

   kuunda timu ili kudhibiti hali hiyo iliyokuwa imeota mizizi, ambapo wafanyabiashara walio wengi ukwepa kupita katika mipaka rasmi.

      Mwenyekiti wa kamati hiyo INNOCENT MADUHU ambaye pia ni kaimu afisa mipango wa wilaya hiyo, amesema wananchi walioko mpakani wana mazoea ya kuuza kahawa na mazao mengine kwa wanunuzi wasio rasmi, ambao hutorosha bidhaa hizo nje ya nchi kupitia mto Kagera, unaotenganisha nchini ya Tanzania na Uganda.

      Katika zoezi hilo mbali na kukamatwa kwa zaidi ya tani tano za kahawa, pia vitu mbalimbali ikiwemo pikipiki kumi, baiskeli na mitumbwi iliyokuwa ikisafirisha bidhaa hizo,pia vilikamatwa.

JIJI LA ARUSHA KUANZA KUPANGWA AGOSTI

   MKURUGENZI Msaidizi wa Mpango Kabambe kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Amulike Mahenge amesema kuwa utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Jiji la Arusha na viunga vyake unatarajia kukamilika Agosti mwaka huu.

     Kutokana na kukamilika huko, utaanza utekelezaji wake rasmi wa jiji hilo kupangwa kisasa Agosti hiyohiyo. Mahenge alisema mpango huo uliopo katika rasimu ya mwisho ya Mpango Kabambe wa Jiji la Arusha umewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo madiwani.

    Hatua hiyo ni njia ya kuwezesha kupitisha kwenye vikao vya Baraza la Madiwani na hatimaye kupitiwa na Mkurugenzi wa Miji Wizarani kwa ajili ya kuanza kujengwa mji wa kisasa jijini Arusha na katika viunga vyake.

    Mahenge aliyasema hayo jana, jijini hapa alipozungumza na wadau wa maendeleo waliokutana kwa pamoja kwa ajili ya kuchangia mada na kuona jinsi Mji wa Arusha utakavyokuwa wa kisasa.

   Alisema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itapitia mpango huo mara baada ya madiwani kupitisha kwenye vikao vyao vya mabaraza, kisha utekelezaji wake utaanza rasmi Agosti mwaka huu.

    “Mpango huu ni Mpango Kabambe utakaobadilisha taswira ya Jiji la Arusha na halmashauri zake hivyo ni vyema wadau wa maendeleo wakapitia mpango huu na kujadili kwa kina ili kuona Arusha,” alisema Mahenge.

    Naye Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega akifungua mkutano huo aliwasihi kuhakikisha wanajadili kwa kina jinsi ya kupanga mji, pamoja na kutoa mawazo yao pale wanapoona kuna mahali pa kurekebishwa kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Madiwani ili kupitishwa na kuanza rasmi.

   Alisema eneo lililoandaliwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo ni kilometa za mraba 608; Halmashauri ya Jiji la Arusha zipo kilometa za mraba 272 na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na Meru zitahusika kilometa za mraba 187.

   Alisema zaidi ya Sh bilioni nane zimetumika kuhakikisha majiji mawili ya Arusha na Mwanza yanapangwa vizuri hasa kutokana miji hiyo kukua kwa kasi.

   Mwaka juzi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilisaini mkataba wa makubaliano na Kampuni ya Subrana International Pty Ltd ya nchini Singapore, kwa ajili ya kuendeleza majiji mawili ya Arusha na Mwanza na unatakiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Dkt. TULIA AWAKINAI UKAWA

  Naibu Spika, Dk Tulia Ackson  Dodoma.

   Naibu Spika, Dk Tulia Ackson leo ameonekana kuchoka kitendo cha wabunge wa Ukawa kususia vikao vyake na kuwataka watoke haraka bungeni kama hawahitaji kuendelea na kikao. Dk Tulia amesema hayo wakati wabunge hao walipoanza kutoka bungeni baada ya dua.

    Amewataka watoke haraka kwa sababu walikuwa wanachelewesha shughuli za Bunge.

      Leo ni siku ya 19 wabunge hao wanasusia vikao hivyo vinavyoendeshwa na Dk Tulia, juzi walitangaza kuvunja uhusiano wa kawaida na wabunge wa CCM jambo ambalo limelaaniwa na wawakilishi hao wa chama tawala.

TUMIA PARACHICHI KULAINISHA NGOZI

   VITU vya asili navyo vinasaidia kuweka ngozi kuwa nzuri wakati wowote ule, ngozi ni kiungo kikubwa kwa binadamu hivyo inatakiwa kuwa waangalifu kuitunza ili kuepusha isizurike na kitu kingine chochote.

      Ngozi ni kiungo ambacho kinachopokea magojwa haraka hivyo ndio maana tunaambiwa ni vizuri kuitunza ili isipoteza uasilia wake. Ngozi nzuri ni ile ambayo haijapoteza uasilia wake wakati wote na kila siku uonekana vilevile ilivyo lakini hiyo inatokana na jinsi mtu anavyoweza kuitunza ngozi hiyo.

    Kwa upande wa wanawake tunathamini mno ngozi ya usoni tofauti na sehemu nyingine katika mwili,  kwani ngozi ya uso ni muhimu na vilevile ni rahisi kushika vigonjwa vidogovidogo ambavyo vinavyokuwa vinaharibu ngozi yako.

    Hakuna mwanamke asiyependa ngozi ya sura yake haijarishi kama sura yake ni mbaya au nzuri lakini ilimradi tu  ngozi yake iwe nzuri na safi. Wanawake hutumia pesa nyingi kwa ajili ya kununua vipodozi vya usoni ili kuweka ngozi yake kuwa nzuri wakati wowote ule.

     Lakini vipodozi vingi ambavyo vinavyotumiwa na wanawake vina sumu ya kemikali ambayo wakati mwingine inasababisha kuharibu ngozi ya mtumiaji wa hicho kipodozi.

    Ndio maana wataalam wa masuala ya ngozi wanashauri wanawake kuwa makini katika uchaguzi wa vipodozi wanavyotumia ili wasiweze kudhurika. Ngoja nirudi katika mada yetu ambayo tuliyokusudia leo ya kutumia vitu mbalimbali ambavyo vitakavyowezesha kuwa mrembo zaidi na ngozi kuwa nzuri wakati wote ule.

     Matunda kama parachichi, tango limao, matunda haya mara nyingi ukitumia usoni inakufanya ngozi yako kuwa nzuri na nyororo wakati wowote ule.

    Uzuri wa matunda haya hayana kusema kuwa umekosea masharti au umezidisha dozi matunda haya hata ukipaka kwa wingi usoni kwako haviwezi kuleta athari yeyote katika ngozi yako. Pia mafuta ya mawese nayo nayasaidia kuifanya ngozi yako kuwa laini na kung'aa na vilevile inasaidia kuondoa taka zote zilizokuwa usoni.

      Hata unga wa dengu nao unasaidia kupendezesha sura yako hasa ukichanganya na kiini cha yai ya kuku wa kienyeji. Mafuta ya nazi nayo yanasaidia kuondoa harara usoni na kuifanya sura yako ipendeze wakati wote, hivyo vitu kama hivi mara nyingi vinasaidia kutoondoa uasili wa rangi ya ngozi yako siku zote. Wapo wanawake wanaotumia vitu vaya asili na ukiwaona sura zao huwa ni nzuri wakati wote na wanakuwa hawabadili uasili wa ngozi yao .

VvKama ni mweupe utakuwa ni mweupe vilevile ila atakuwa anaufanya weupe wake uwe na thamani kwani wakati wote atakuwa anang'ara na kupendeza. Na kama mweusi atabaki na rangi yake hiyo hiyo ila itakuwa ni mweusi wa kupenda na kila wakati utakuwa unamtamani kwa sababu ya rangi yake ya asili.

    Urembo wa asili uanaweza kutumiwa hata na watoto waliochini ya miaka 18 kwa kuwa haudhuru ngozi na kutosabisha magojwa ya ngozi. Vipodozi vyenye kemikali mara nyingi husababisha kupotea kwa rangi yako asilia na vilevile husababisha ugojwa wa saratani ya ngozi ambayo mwisho wake husababisha kifo.

TANZANIA NA UGANDA WATAKIWA KUSITISHA UWINDAJI

  Arusha.

Serikali ya Tanzania na Uganda, zimeshauriwa kusitisha kwa muda uwindaji wa kitalii wa tembo ili kudhibiti matukio ya ujangili ambayo yanaendelea kupunguza idadi ya wanyama hao duniani.

   Mkurugenzi wa Taasisi ya Elephant Neighbors Center ya Kenya, Jim Nyamu ametoa wito huo wakati akiongoza matembezi ya kilomita 3,200 katika nchi za Afrika ya Mashariki kupinga mauaji ya tembo ambayo yamefika Arusha.

  Matembezi hayo yameanzia Nairobi Kenya kwa kuzinduliwa na Mke wa Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta, Margaret na yanatarajiwa kufika jijini Dar es Salaam Julai 6 na kupokewa na Mke wa Rais John Magufuli, Janeth  na baadaye kuendelea nchini Uganda.

YOUNG D AKIRI ALIKUWA ANATUMIA MADAWA YA KULEVYA ,AOMBA MSAMAHA AHAIDI MAISHA MAPYA

   Rapper Young Dee hatimaye amethibitisha tetesi za miaka mingi kuhusu utumiaji wa madawa ya kulevya na kukiri kuwa ametumia kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

    Akiongea na waandishi wa habari leo, Escape One jijini Dar es Salaam, rapper huyo amewaomba radhi watanzania kwa vitendo hivyo na kuahidi kubadilika. Amedai kuwa ni marafiki ndio waliompoteza na kumuingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.

    Amesema amepewa ushauri nasaha na wataalam na kwamba ameachana na matumizi hayo. Pia rapper huyo amerejea rasmi kwenye uongozi wake wa zamani, Million Dollar Boyz, MDB alioachana nao mwaka jana.

     Young Dee na meneja wake Max Rioba Kwa muda mrefu rapper huyo alikuwa akikanusha tetesi hizo. Taarifa zaidi zitakuja punde.

WATU 80 WAUAWA NCHINI INDIA

India radi Maafisa nchini India wanasema kuwa watu 80 wameuwawa baada ya kupigwa na radi katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa taifa hilo katika muda wa saa 24 iliyopita.

    Watu 53 walifariki katika jimbo la Bihar.Watu 10 waliuawa katika jimbo la mashariki la Jharkhand huku wengine 16 wakifariki katika eneo la Madhya Pradesh.

    Wengi waliuawa walipokuwa wakifanya kazi katika mashamba yao wakati huu wa msimu wa mvua Ni idadi kubwa sana ya watu kuuawa kwa mpigo mmoja ,jambo ambalo limewashangaza wengi. Katika muongo uliopita, zaidi ya watu elfu mbili wamefariki kwa kupigwa na radi kote nchini India.

    Ni vigumu sana kubashiri ni lini janga la radi litatokea na si rahisi kwa utawala kutoa tahadhari ya kutokea kwa radi.

IVO MAPUNDA AKUNJA VIRAGO AZAM FC

    Azam FC imeamua kuachana na kipa wake mkongwe Ivo Mapunda waliyemsajili msimu uliopita kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake, huku wakifanya mchakato wa kumsajili kipa mwingine.

   Ivo ambaye ni kipa mkongwe alitua Azam FC msimu uliopita akitokea Simba baada ya kushindwa kumsajili katika dakika za mwisho ambapo wanalambalamba hao waliamua kumpa mkataba wa mwaka mmoja. Katibu Mkuu wa Azam FC, Idrisa Nassor amesema kuwa, hawataendelea na Ivo msimu ujao wa ligi kuu na kwa sasa wanafanya mchakato wa kusajili kipa mwingine atakayeziba nafasi yake.

     “Hatutarajii kuendelea na Ivo msimu ujao wa ligi kuu na badala yake nafasi yake itachukuliwa na kipa mwingine ambaye tunafanya mchakato wa kumsajili ili kuziba nafasi hiyo.

    “Kwa sasa amebakiza miezi mitatu ili kukamilisha mkataba wake na Azam aliosaini mwaka mmoja msimu uliopita na baada ya hapo tutaangana alisema bosi huyo.

IBRAHIMMOVIC KUSTAAFU SOKA YA KIMATAIFA

   Ibrahimovic Nyota wa Sweden Zlatan Ibrahimovich ametangaza kwamba atastaafu katika soka ya kimataifa baada ya michuano ya Euro 2016.

    Taifa lake linakutana na Ubelgiji katika mechi ya mwisho ya kundi E siku ya jumatanoambayo huenda ikawa mechi yake ya mwisho kwa taifa lake. Alisema:Ninajivunia kile nilichofanikiwa kupata na kila mara nitatembea na bendera ya Sweden.

     Klabu ya Manchester United imehusishwa pakubwa na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye alikuwa ajenti huru baada ya kuondoka klabu ya Paris Saint Germain ya Ufaransa .

WASOMI WAPONGEZA RAISI KUKATWA KODI

UAMUZI wa Serikali wa kuwakata kodi kwenye kiinua mgongo chao viongozi wa kisiasa akiwemo Rais John Magufuli, umepongezwa na wasomi na wanasiasa, wakieleza unaleta usawa katika jamii.

     Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema ilikuwa ni mazoea mabaya kuwaacha viongozi wanasiasa kutolipa kodi wakati wanapomaliza muda wao; wakati watumishi wa kawaida ambao vipato vyao ni vidogo walikuwa wanakatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, alisema uamuzi huo umeifanya serikali kuwa na chanzo kipya cha mapato, lakini pia ni uamuzi ambao umeleta haki katika jamii.

    “Maamuzi haya yalitakiwa kufanywa miaka ya nyuma, niseme tumechelewa sana maana hawa viongozi wanahudumiwa kila kitu na kupatiwa matibabu, ki ukweli wana maisha mazuri. Kitendo cha kuwasamehe kodi kwenye kiinua mgongo chao haikuwa halali,” alisema Profesa Ngowi.

   Alisema hatua hiyo ilikuwa inaongeza pengo la kipato kati ya wananchi wa kawaida na viongozi wa kisiasa, kwani ilikuwa viongozi ambao wana maisha mazuri wanaongezewa faida nyingine ya kutokatwa kodi na mtumishi wa kawaida, ambaye anapata mshahara mdogo alikuwa analipa kodi anapostaafu.

    Hata hivyo alisema matunda ya uamuzi huo wa serikali, yataanza kupatikana baada ya miaka mitano. “Hivyo hakuna fedha itakayoingia mwaka ujao wa fedha hadi mwaka 2020 ndipo serikali itapata kodi hiyo kutoka kwa viongozi wanasiasa wastaafu,” alisema.

   Wasomi kwenye siasa Alisema uamuzi huo wa serikali, pia unaweza kusaidia kupunguza kasi ya wasomi kuingia kwenye siasa maana watafahamu kwamba kuanzia sasa baadhi ya vivutio vilivyokuwepo vinaanza kuondolewa.

    Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kupunguza Umasikini (Repoa), Dk Donald Mmari alisema uamuzi wa viongozi wa kisiasa, kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao ni jambo jema kwa sababu ni kada, ambayo kiinua mgongo chao ni kikubwa na kutokatwa kodi haki haikuwa inatendeka.

Tuesday, June 21, 2016

STAR WA USWIS AFANANISHA JEZI ZAO NA CONDOM

    Puma ambao ni watengenezaji wa jezi za Uswis imesema, wachezaji wa timu hiyo walivaa jezi  zilizokuwa na mapungufu ndiyo maana zilikuwa zikichanika wakati wa mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Ufaransa uliomalizika kwa suluhu.

     Tatizo hilo lilipelekea star wa Uswis Xherdan Shaqiri kusema: “Nadhani Puma hawatengenezi condom.” Kiungo mpya wa Arsenal Granit Xhaka alilazimika kubadili jezi mara mbili,

    wakati Valon Behrami, Admir Mehmedi, Fabian Schar, Breel Embolo na Blerim Dzemaili wao wakibadilisha mara moja baada ya jezi zao kuchanika wakati wa mchezo dhidi ya Ufaransa Kabla ya michuano hiyo kuanza, mshambuliaji Embolo alilazimika kubadili jezi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Montenegro, wakati mshambuliaji huyo wa Basel akasema: “Tumekuwa na tatizo la jezi.

    Kit manager wetu bado hajaliona hilo, lakini sisi tumeshaliona.” Taarifa ya Puma kuomba radhi kwa chama cha soka sha Uswis pamoja na wachezaji ilisema: “hatukutarajia kitu kama hiki.” Puma wamesema, tatizo hilo limeathiri baadhi ya jezitu, ambazo zilichanganywa na elastane na polyester fibers zilizotengenezwa Uturuki.

    Puma wanazalisha jezi kwa nchi tano zinazoshiriki michuano ya Euro 2016 huku Italy ikiwemo.

Monday, June 20, 2016

UGONJWA USIOFAHAMIKA WAUA WATU DODOMA

   Watu saba wamefariki dunia kwenye kijiji cha Chemba, mkoani Dodoma na wengine zaidi ya 14 wamelazwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo kutokana na kukumbwa na ugonjwa usiofahamika.

   Ugonjwa huo umekuja baada ya watu hao kula nyama ya ng’ombe aliyechinjwa na kugaiwa kwa baadhi ya watu kwenye kijiji hiko.

     Mmoja wa mzee wa familia iliyokumbwa na ugonjwa huo amesema, “Tulikula nyama tuliyopewa na jirani yetu na jioni tukala ugali na maziwa. Tulianza kuugua na baada ya siku tatu kutapika na kuharisha.”

    Dalili za ugonjwa huo ni kutapika,kuharisha,kupata rangi ya manjano machoni na sehemu zingine na tumbo kuvimba na kujaa maji. Lakini pia ugonjwa huo umeuwa paka pamoja na mbwa ambao walikula nyama hiyo.

    Muuguzi wa hospitali hiyo, Stella Joseph amemweleza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu kuwa wamepowapokea wagonjwa hao wakiwa wanaharisha na kutapika, lakini kwa sasa wamefunga.

   Waziri wa Afya Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto mhe Ummy Mwalimu amesema tayari sampuli za ugonjwa huo zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa serikali kwa ajili ya uchunguzi huku akiwatoa hofu wakazi wa mkoa huo ambao wanahisi huenda ukawa ni ugonjwa wa kimeta.

FAMILIA YAINGILIA KATI ISHU YA MWANAUME 'TATA' KUMTAKA JUX

   DAR ES SALAAM: Familia ya staa wa Bongo Fleva, Juma Musa ‘Jux’ imeingilia kati ishu ya mwanaume ‘tata’, mkazi wa Dar, James Delicious aliyetangaza kumtaka kimapenzi msanii huyo ambaye ni mpenzi wa Mwanamuziki Vanessa Mdee ‘V-Money’.

   Akizungumza na Wikienda kwa niaba ya familia, dada wa Jux, Fatu-ma Juma alisema kuwa hakuna kitu kinachowaudhi kama kijana huyo kutwa kutangaza kumpenda na

  
    kumtaka mdogo wao huyo wakati wote ni wanaume na ni kinyume cha maadili ya kidini (familia ya Kiislam), Kitanzania na Kiafrika kwa jumla.

     “Kiukweli familia inachukizwa sana na tabia ya huyo kijana ambaye haoni aibu, tunamtaka kuacha mara moja kusumbua watu akitaka namba ya Jux la sivyo tutachukua hatua za kisheria kwani anatukera sana,” alisema Fatuma.

    Hivi karibuni kijana huyo alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa lazima ampindue Vanessa kwa Jux kwani anampenda jamaa huyo kupita kiasi.

Wednesday, June 15, 2016

TRUMP ASISITIZA WAISLAMU WASIINGIE MAREKANI

   MGOMBEA wa kiti cha urais wa kupitia chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump, amesisitiza kuwa, mauaji ya watu 50 yaliyotokea kwenye Klabu ya wapenzi wa jinsia moja, yamethibitisha msimamo wake wa kutaka waislamu wapigwe marufuku kuingia humo.


    Katika hotuba yake kwenye jimbo la New Hampshire, Trump amesema mfumo wa Idara ya uhamiaji nchini Marekani, umeruhusu familia ya Omar Marteen, aliyetekeleza mauaji hayo kuingia nchini Marekani.

    Alidai kuwa, bado mfumo huo umeendelea kuruhusu wauaji wengine kuingia nchini humo bila vikwazo. Alisema, sababu moja wapo inayochochea muuaji kuwepo nchini Marekani, ni familia ya Marteen kuingia nchini humo.

    Aliongeza kuwa, mfumo wa idara ya uhamiaji isiyotekeleza wajibu wake, bado hairuhusu kujua ni nani anayepaswa kuingia Marekani ili raia wa nchi hiyo walindwe. Kwa upande wa Mgombea urais kupitia Democratic, Hillary Clinton, akitoa risala za pole kwa waathiriwa wa mkasa huo, alisema Trump ni kama mtoto anayesema ovyo kwa namna anavyougeuza mkasa huo wa kitaifa kujipongeza binafsi.

     Akizungumza jimboni Ohio, Hillary, amekosoa mpango wa mpinzani wake ambaye ni Trump, kuwazuia waislamu kuingia Marekani “Hatua hiyo ya uchochezi ya vitisho kuzuia familia na marafi ki wa kiislamu kuingia marekani, pia mamilioni ya wafanyabiashara na watalii waislamu kuingia nchini, inaumiza sehemu kubwa ya waislamu wanaopenda uhuru na kuchukia ugaidi,” alisisitiza.

    Naye Rais wa Marekani, Barack Obama alisema, hakuna ushahidi kuwa aliyetekeleza mashambulizi hayo alikuwa sehemu ya mpango mkubwa wa mashambulizi. Obama alieleza kwamba, shambulio hilo lilisukumwa na msimamo binafsi wa mshambuliaji huyo na hakuna ushahidi kuwa, Marteen alipata maelekezo kutoka nje ya nchi kutekeleza mauaji. Lakini, Mkurugenzi wa shirika la kijasusi la FBI,James Comey, alisema kuna ishara kuwa Marteen alishawishika kupitia mitandao ya intaneti ila bado haijajulikana kama kijana huyo alikuwa anaunga mkono kundi gani la kigaidi.

    Comey alisema, muuaji huyo alieleza kuunga mkono kundi la wanamgambo wa Dola ya Kiislamu (IS) pamoja na kundi hasimu na IS la Al Nusra kutoka nchini Syria. Katika hatua nyingine,Silaha mbili zilizotumiwa na Marteen zimebainika kununuliwa kwenye kituo cha kuuza silaha.

     Mmiliki wa duka hilo Edward Henson, alisema Marteen alipitia taratibu zote zinazopaswa kufuatwa wakati wa kununua silaha hizo. Naye mke wa zamani wa Marteen, Sitora Yusufi y, amemwelezea mumewe kama mtu aliyekuwa na tabia za ugomvi ya kutaka kupiga watu lakini hakuwa na itikadi kali za kidini.

    Tukio hilo lililohusisha mauaji ya watu 50 na kujeruhi wengine zaidi ya 53 yalitekea kwenye klabu ya starehe ya mashoga iliyopo Frolida Jumapili ya wiki iliyopita. Marteen,alivamia kwenye klabu hiyo kisha kuwafyatulia risasi mfululizo watu waliokuwepo ndani. Wakati akitekeleza mauaji hayo, Marteen aliwateka nyara watu wengine zaidi ya 30 ambao waliokolewa na polisi.

    Mtuhumiwa huyo ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi, ilielezwa alishawahi kuhojiwa na maofisa usalama mwaka 2013 na 2014 akihusishwa na makundi ya kigaidi.