Monday, June 13, 2016

HOSPITALI YA KISASA CHANIKA KUGHARIMU SH 18 BILLIONI

   Dar es Salaam. Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Korea (Koica)  inatarajia kutumia Sh18 bilioni kukamilisha Ujenzi wa Hospitali ya kisasa kwa ajili ya huduma za mama na mtoto katika Kata ya Chanika, wilayani humo.

    Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk Meshack Simwela amesema kuwa hospitali hiyo itakapokamilika itakuwa na vifaa vya kisasa pamoja na madaktari bingwa kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, Amana, Mnazi Mmoja pamoja na hospitali nyingine za Serikali.

  
     “Mpaka sasa jumla ya waganga watano na wauguzi sita wameshapelekwa Korea kujifunza namna ya kutoa huduma na jinsi ya kutumia vifaa vipya vitakavyoletwa mara baada ya Hospitali hii kukamilika,” amesema Dk Simwela.

     Akizungumzia maboresho yanayofanywa katika Sekta ya Afya ndani ya Manispaa hiyo, Ofisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, David Langa amesema hospitali hiyo itakayokuwa na vitanda 266 pamoja na mashine zote za upasuaji itakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

No comments:

Post a Comment