Thursday, June 23, 2016

IBRAHIMOVIC ASTAAFU RASMI SOKA LA KIMATAIFA

   Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic amestaafu rasmi kuitumikia timu yake ya taifa ya Sweden ambapo jana timu yake iliondolewa kwenye michuano ya Euro 2016 baada ya kufungwa 1-0 na Ubelgiji na huo kuwa mchezo wake wa mwisho.

       Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34, siku ya Jumanne wiki hii, alitangaza kuwa michuano ya Euro 2016 itakuwa michuano yake ya mwisho kuitumikia timu yake ya taifa. Alifunga mabao 62 katika michezo 116, lakini alishindwa kutikisa wavu katika Euro mwaka huu.

        Aidha, Ibrahimovic hataiwakilisha tena nchi yake katika Rio Olimpiki kama ilivyokuwa imefikiriwa hapo awali. Kocha wa Sweden, Erik Hamren amesema, "Katika nchi ndogo kama Sweden, huwezi kupata mchezaji mwingine kama yeye, kweli yeye ni wa kipekee."

        Sweden haikufanikiwa kuishinda timu yoyote kwenye kundi E, katika mechi yake na Ireland ilitoka sare ya 1-1 na kupoteza michezo yote ya Italia na Ubelgiji.

     Mshambuliaji huyo wa zamani wa Ajax, Barcelona, Juventus na Inter Milan amekuwa akihusishwa kuhamia Manchester United tangu kuamua kuondoka Paris St-Germain.

No comments:

Post a Comment