Tuesday, June 7, 2016

MUUGUZI UGANDA AZIMIA GHAFLA AKIHUDUMIA WAGONJWA WODINI

  Kampala. Uganda. Baadhi ya wagonjwa katika Kituo cha afya cha Nakapiripiri1V kilichopo wilayani Karamoja, kaskazini mashariki mwa Uganda juzi walikumbwa na butwaa baada ya muuguzi aliyekuwa akiwahudumia, kuzimia ghafla.

    Muuguzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kwa hofu ya kukumbwa na vitendo vya unyanyapaa, alikuwa akihudumia wodi mbili ambazo moja ilikuwa ya upasuaji na nyingine ya uzazi. Muuguzi huyo alikumbwa na masahibu hayo wakati akimsaidia daktari moja aliyekuwa akiendesha operesheni kuokoa maisha ya mjamzito na mwanaye wakati wa kujifungua.

    Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. John Anguzu ambaye aliendesha operesheni hiyo alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo akisema kuwa muuguzi huyo alikuwa hajala chakula tangu aingie kazini. Hata hivyo, hakubainisha muda alioingia kazini muuguzi huyo mbali ya kuelezea mazingira ya tukio hilo.

    “Alikuwa akinisaidia katika chumba cha upasuaji na kile alichokuwa akitakiwa kufanya ni kuniletea vifaa vyote vilivyokuwa vinatakiwa katika operesheni. Pia, alikuwa akinisaidia kushika tochi tuliyokuwa tukitumia kwa vile mashine yetu ya sola tunayotumia siku zote ilikuwa haifanyi kazi.

    “Wakati tunaendelea na kazi yetu mle wodini ghafla alilalamika kuashiria kutaka msaada na baadaye akaanguka,” alisema daktari huyo. Dk Anguza alisema pamoja na tukio hilo, lakini alifanikiwa kufanikisha operesheni kuokoa maisha ya mama na mtoto akisaidiwa na wauguzi wengine na baadaye kumsaidia muuguzi huyo aliyezimia.

  '' Tulifanikiwa kuwahudumia wote na sasa wanaendelea vyema kwani baada ya tukio hilo walikuja wauguzi wengine ambao tulisaidiana vyema kumwokoa mama na mtoto wake na kisha kumsaidia muuguzi aliyekuwa amezimia,” alisema daktari huyo. Dk Anguza alisema, muuguzi huyo ni miongoni mwa wakunga waliohitimu mafunzo yaliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA).

    “Anaipenda kazi yake na bahati mbaya kile kilichomtokea siku ile ni kwa sababu ya njaa. Alikuwa hajala kitu chochote tangu aingia kazini,” alisema. UNFPA imekuwa ikiendesha program mbalimbali za kutoa mafunzo maalumu kwa wakunga ili kuondokana na tatizo la wataalamu wa kadi hiyo.

    Umoja wa Matifa ulisema hivi karibuni kuwa moja ya mambo yanayosababisha kuwapo kwa ongezeko la vifo vya kina mama wakati wa kujifungua ni kutokana na kukosekana kwa wataalamu wa kutosha ikiwamo wakunga.

  
   Nchi za Afrika Mashariki zinatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zinakabiliwa na upungufu wa wakunga hatua ambayo imelazimu baadhi ya mashirika ya kimataifa kuanzisha mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.

   Hivi karibuni UNFPA ilitangaza kuanzisha programu maalumu inayozilenga nchi za Tanzania, Kenya Rwanda na Uganda kwa ajili ya kuwaandaa wakunga watakao toa huduma ya kisasa kwa wagonjwa kwenye nchi zao.

No comments:

Post a Comment