UAMUZI wa Serikali wa kuwakata kodi kwenye kiinua mgongo chao viongozi wa kisiasa akiwemo Rais John Magufuli, umepongezwa na wasomi na wanasiasa, wakieleza unaleta usawa katika jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema ilikuwa ni mazoea mabaya kuwaacha viongozi wanasiasa kutolipa kodi wakati wanapomaliza muda wao; wakati watumishi wa kawaida ambao vipato vyao ni vidogo walikuwa wanakatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, alisema uamuzi huo umeifanya serikali kuwa na chanzo kipya cha mapato, lakini pia ni uamuzi ambao umeleta haki katika jamii.
“Maamuzi haya yalitakiwa kufanywa miaka ya nyuma, niseme tumechelewa sana maana hawa viongozi wanahudumiwa kila kitu na kupatiwa matibabu, ki ukweli wana maisha mazuri. Kitendo cha kuwasamehe kodi kwenye kiinua mgongo chao haikuwa halali,” alisema Profesa Ngowi.
Alisema hatua hiyo ilikuwa inaongeza pengo la kipato kati ya wananchi wa kawaida na viongozi wa kisiasa, kwani ilikuwa viongozi ambao wana maisha mazuri wanaongezewa faida nyingine ya kutokatwa kodi na mtumishi wa kawaida, ambaye anapata mshahara mdogo alikuwa analipa kodi anapostaafu.
Hata hivyo alisema matunda ya uamuzi huo wa serikali, yataanza kupatikana baada ya miaka mitano. “Hivyo hakuna fedha itakayoingia mwaka ujao wa fedha hadi mwaka 2020 ndipo serikali itapata kodi hiyo kutoka kwa viongozi wanasiasa wastaafu,” alisema.
Wasomi kwenye siasa Alisema uamuzi huo wa serikali, pia unaweza kusaidia kupunguza kasi ya wasomi kuingia kwenye siasa maana watafahamu kwamba kuanzia sasa baadhi ya vivutio vilivyokuwepo vinaanza kuondolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kupunguza Umasikini (Repoa), Dk Donald Mmari alisema uamuzi wa viongozi wa kisiasa, kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao ni jambo jema kwa sababu ni kada, ambayo kiinua mgongo chao ni kikubwa na kutokatwa kodi haki haikuwa inatendeka.
No comments:
Post a Comment