Tanzania imekuwa ikipoteza zaidi ya shilingi bilioni 300 kila mwaka kutokana na kutokusimamiwa vizuri kwa makusanyo ya mapato yanayotokana na sekta ya mkaa unaotumika katika miji mbalimbali nchini na kusababisha uharibifu mkubwa wa misitu ya asili ambayo ina umuhimu mkubwa kwa uchumi na maendeleo ya taifa.
Hayo yamesemwa mjini Dodoma na mwenyekiti mpya wa bodi ya taasisi ya utafiti wa misitu nchini tafori wakati akiwasilisha mada kwenye mkutano wa wajumbe wa kamati za bunge za ardhi maliasili na utalii na nishati na madini ulioandaliwa na mtandao wa jamii wa usimamizi wa misitu nchini Mjumita na ameishauri serikali kutokuiweka sekta ya misitu katika mipango ya makusanyo ya fedha kwani kufanya hivyo kunachochea uharibifu wa misitu kwa wakala wa huduma za misitu nchini Tfs ambao wamewekewa malengo ya kukusanya fedha badala ya kusimamia uhifadhi wa misitu.
Nao baadhi ya wabunge wa kamati hizo wameishauri serikali kupiga marufuku matumizi ya mkaa katika miji mikubwa na majiji kwa kuanzia na jiji la Dar es Salaam ambalo linaongoza kwa matumizi ya mkaa mwingi na iwekewe mipango ya kutumia nishati mbadala kama gesi na mkaa endelevu lakini pia wameshauri juhudi za kukabiliana na athari za kimazingira ziendane na mipango na sera ya kuhimiza uzazi wa mpango kama njia ya kupunguza ongezeko la watu linalochochea uharibifu wa misitu na mazingira kote nchini.
No comments:
Post a Comment