Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.
Ummy Mwalimu amesema sensa ya kitaifa ya mwaka 2012 inaonesha kuwa wanawake 432 kwa kila vizazi hai laki moja hufariki dunia kila mwaka kutokana na matatizo yatokanayo na uzazi.
Amesema miongoni mwa matatizo hayo ni pamoja na kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua. Mhe. Ummy ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya siku ya wakunga duniani, ambayo inaadhimishwa tarehe 5 ya mwezi wa 5 kwa kila mwaka. Amesema kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua huchangia vifo asilimia 25, uzazi pingamizi asilimia 11 na maambukizi vifo asilimia 11.
Amesema sababu nyingine zinazochangia vifo ni pamoja na ukosefu wa damu, Malaria na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Amesema sekta ya afya ni moja ya sekta zilizo kwenye mpango wa matokeo makubwa sasa BRN hivyo ni lazima kujirekebisha katika makosa mbalimbali na wale wachache wanaoharibu lazima wabainishwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake Rais wa chama cha wakunga nchini Bi Teddy Mwanga amesema tayari wameanza kuwachukulia hatua za kisheria wakunga wote wanaolalamikiwa kwa kuwafanyia vitendo vya ukatili wagonjwa pindi waendapo kupatiwa huduma ya kuzalishwa.
Nao baadhi ya wakunga waliopewa zawadi ya utumishi bora katika utendaji wao wa kazi za kuwahudumia wanawake wajawazito nchini wameiomba jamii ya watanzania kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja ili kuboresha huduma ya afya kwa mama na mtoto.
Maadhimisho ya siku ya wakunga duniani mwaka huu nchini Tanzania yalikuwa na kauli mbiu isemayo "Wanawake na watoto wachanga ni muhimili wa ukunga".
No comments:
Post a Comment