Wednesday, June 1, 2016

WANAKIJIJI IPERA ASILIA WATAKA UFUMBUZI JUU YA MIGOGORO

Morogoro. Wananchi wa Kijiji cha Ipera Asilia wilayani Malinyi wameuomba uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Morogoro kuunda kamati maalumu ya uchunguzi ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa wafugaji na wakulima uliosababisha kifo cha mtu mmoja.

    Wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji  hicho wananchi hao wamesema wanaiomba Serikali ya Mkoa wa Morogoro kuwaondoa wakulima katika eneo hilo kwani ni eneo la mifugo.

   Mmoja wa wananchi hao, Mipawa Chibubu Jilala (80) amesema kuwa Serikali inapaswa kuingilia kati na kuwaondoa wakulima waliovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo.

  “Huu mgogoro mwaka jana ulisababisha mtoto wa mdogo wangu, Jilungu Ilindilo (28) kufa kwa kupigwa risasi tumboni lakini ili amani iendelee kudumu serikali iingilie kati na kuwatoa wakulima kwa nguvu kwani serikali ya wilaya na mbunge wameshindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hili,” amesema Chibubu Jilala.

No comments:

Post a Comment